Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Sisi wajumbe wa Asasi za kiraia za ki-Tanzania tuliokutana leo ukumbi wa Dar es Salaam International Conference Centre, tarehe 10 Machi 2009 kwa uratibu wa mtandao wa Policy Forum, Human Development Trust na Tanzania AIDs Forum, baada ya kujadili na kutafakari kwa kina taarifa za ''mafanikio'' ya utekelezaji mipango ya IMF na sera za Tanzania ki-uchumi kwa miaka ya 2000 hadi 2008 tumebaini yafuatayo:-

1. Ni kweli takwimu zinaonesha kukua kwa uchumi kwa wastani wa zaidi ya asilimia 7% kwa kipindi tajwa,

2. Kukua huku kwa uchumi hakuendani kabisa na kupungua kwa umasikini nchini: wakati uchumi umekua umasikini nao umeonekana kupungua kwa kiasi cha asilimia 1.2 jambo ambalo likitafsiriwa kwa idadi umasikini umeonekana kuongezeka kwa wananchi toka 11.5 milioni mwaka 2001 hadi 13.7 milioni mwaka 2007.

3. Uchambuzi wa kina umebaini pia kuwa kuna pengo kubwa kati ya ''Walionacho'' na ''Wasionacho'', na pengo hili limekua likiongezeka mwaka hadi mwaka.Iwapo serikali haitokuwa makini katika hili uwezekano ni mkubwa kwa nchi kuingia katika machafuko yanayotokana na kukata tamaa kwa wananchi walio na kipato cha chini.

4. Ushauri wa IMF umeibana serikali na kuilemaza hadi kushindwa kutumia wataalamu wake katika kuimarisha uchumi wa nchi na kuhudumia wananchi katika kupunguza umasikini,

5. Kwa ushauri wa IMF, wadau wa ndani wa nchi, zikiwemo AZAKI hazishirikishwi ipasavyo katika kutunga, kuridhia, kusimamia na kutathmini sera za uchumi wa nchi. Jambo hili limefanya Sera kubaki kuwa hodhi ya IMF na Serikali na sio mali ya wananchi.

6. Mfumo huu wa kutengeneza na kusimamia sera umeifanya serikali kuwajibika kwa IMF na Wafadhili/wadau wa maendeleo zaidi kuliko kwa wananchi wake. Suala hili limeathiri hata uwajibikaji katika ngazi za serikali za mitaa. AZAKI, pamoja na taarifa hizi pia imepitia matamko na habari mbalimbali zilizotolewa na viongozi wa IMF zinazosisitiza kuwa IMF ni chombo kinachosisitiza Uwazi na Ushirikishaji wadau katika utendaji wake na kuwa inazitaka nchi washirika wake kuzingatia zaidi ushauri wa wataalamu wa ndani ya nchi zenyewe, sisi tumeazimia mambo yafuatayo:-

1. IMF ishirikishe wadau katika kutunga sera zake kwa nchi husika: suala la IMF kuwa na sera za jumla kwa makundi mbalimbali ya nchi haisaidii kwa kuwa nchi hizi zina mazingira tofauti tofauti. Kwa kuzingatia maoni ya wadau IMF ipunguze/ ilegeze masharti yake katika nchi na kushauri nchi kuunda sera ambazo zinakidhi mahitaji ya watu wake. Kwa mfano, IMF iruhusu serikali itumie fedha toka kwe wafadhili kuwekeza katika miradi ya maendeleo nchini baadala ya kuzitumia kuongeza Akiba ya Fedha za nje.

2. Serikali ya Tanzania ibadili mtazamo wake kwa wadau wa maendeleo; haswa iweke kipaumbele kwa kutumia wadau wake wa ndani, zikiwemo AZAKI katika kutunga, kuridhia, kusimamia na kutathimini sera za uchumi wa nchi. Jambo hili litazifanya Sera kuwa mali ya wananchi. Kuwepo kwa ushirikishwaji katika ngazi mbalimbali ili mipango iweze kukidhi mahitaji ya watu mbalimbali. Kwa mfano, Katika Mpango wa pamoja” Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania 'MPAMITA 2006' a kifungu cha 5 ambao unaangalia na kusimamia kupambana na umaskini.

3. IMF itoe msaada wa kitaalamu kwa serikali ambao unalenga katika kuiwezesha nchi kufanya maamuzi yake yenyewe.

4. IMF isikilize, ipokee na kufanyia kazi ushauri na matakwa ya wananchi katika nchi husika kupitia kwa serikali zao na wadau wengine wa maendeleo wa ndani ya nchi. Kwa mfano, fedha zilizopo katika mabenki, taasisi za fedha na mifuko ya Amana ya Wafanyakazi, zingeliweza kutumika katika kuwekeza katika miradi ya maendeleo baadala ya sasa ambapo IMF inazuia serikali kutumia fedha hizo. Kutokana na sera hii ya IMF na masharti dhidi ya ukopeshaji wa ndani, riba za mabenki kwa mikopo ni kubwa sana kati ya 21 – 25% na kufanya wananchi kushindwa kukopa. Miradi inayoathirika zaidi ni pamoja na Kilimo na Ujenzi wa makazi. Katika nchi yenye kutegemea Kilimo kama Tanzania, sisi tunapendekeza kwamba wataalamu wetu waangalie hali halisi ya uchumi nchini mwetu.