Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

"Kufanikiwa Kuwa na Serikali Yenye Uwazi Kunahitaji Nchi Iweke Mifumo na Mipango Inayohitaji Kuakisiwa Katika Sera, Sheria na Taasisi za Taifa.” Jakaya Kikwete, 2013

Usuli

Mikataba inayoingiwa kati ya mataifa yenye utajiri wa rasilimali na makampuni ya kimataifa ni ya muhimu kwa kuwa inaeleza waziwazi, wajibu, manufaa, haki  na usalama katika  uwekezaji kwenye mafuta, gesi na uchimbaji madini. Kwa miongo mingi sasa, Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi nchini Tanzania umebaki kuwa ni changamoto. Hali hii inazuia wananchi wasiweze kupata taarifa sahihi, na kwa wakati, hili linapunguza hali ya kujiona kuwa ni wamiliki wa rasilimali zao na kunapunguza shauku na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika majadiliano na maamuzi kuhusu usimamiaji wa rasilimali za umma. Kuna tofauti kati ya Uwazi wa Mikataba na Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi. Uwazi wa Mikataba ni uwekaji na upatikanaji rahisi wa mikataba inayohusu rasilimali za umma iliyoingiwa kati ya serikali na makampuni. Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi ni kuhusu kuufanya mchakato wote wa utayarishaji wa mikataba kuwa wazi, wa haki, na wenye ufanisi: tokea hatua za upangaji, utoaji wa zabuni, ugawaji linganifu, na utoaji wa mikataba hadi utekelezaji.

Wajibu wa Watunga Sera na Wananchi

Watunga sera na Wananchi wanawajibu wa kufanikisha suala la Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi.

Watunga sera wana wajibu ufuatao:

  • Kupigania upatikanaji wa sheria au Ibara mahususi inayohusiana na Uwekaji Wazi wa mwenendo waUpatikanaji wa Mikataba;
  • Kuanzisha jopo la watunga sera (hasa wabunge) litakalojikita katika masuala ya mikataba;
  • Kujenga mahusiano na waandishi wa habari ili kuinua uelewa wa umma kuhusu Uwekaji Wazi wa mwenendo waUpatikanaji wa Mikataba na kuonyesha maeneo ambapo mchakato unaweza kuboreshwa;
  • Kufanya kazi kwa pamoja na AZAKI zinazojihusisha na masuala ya Uwekaji Wazi wa mwenendo waUpatikanaji wa Mikataba na uziduaji;

Wananchi wanawajibu ufuatao:

  • Kudai taarifa kuhusu utayarishaji wa mikataba ya umma; muundo wa uendeshaji shughuli, mapato, tathmini ya matokeo kwa mazingira na mgawanyo wa mapato.
  • Kushiriki kikamilifu katika majadiliano na maamuzi yanayofanywa kwenye sekta ya madini, mafuta na gesi

Usimamizi na Utoaji wa Mikataba Nchini

Taasisi kuu inayowajibika kwa viwango na taratibu za ununuzi wa umma na inayofuatilia mashirika/taasisi za ununuzi wa umma kama zinafuata kanuni zilizowekwa ni Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).  Shirika la Huduma za Manunuzi ya Serikali (GPSA) hufanya ununuzi wa jumla kwa makadirio ya mahitaji ya taifa kwa lengo la kuuza tena kwa taasisi za serikali na zisizo za kiserikali. GPSA huchapisha data za manunuzi katika tovuti yake kwa muundo wa data za wazi.

Serikali imekuwa ikisimamia utekelezaji wa viwango na taratibu za manunuzi ya umma lakini, hakuna mpango ulio wazi wa kuhakikisha kuna Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi

Mfumo wa kisheria unaoongoza PPRA hautoshelezi. Marekebisho ya sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2016, yana madhumuni ya kushughulikia mapengo ya kisheria ikiwa ni pamoja na uwepo wa shahidi wakati wa kutia sahihi mikataba, na kwa vyombo/taasisi husika kutoa taarifa za manunuzi kwa njia ya kielektroniki (inapowezekana) au kwa mkono.  Sheria ya Manunuzi ya Umma ya 2016, inatakiwa iguse na maeneo mengine zaidi ya kuwa na shahidi, inatakiwa igusie pia suala la Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi. Sheria nyingine zinazozungumzia upatikanaji wa taarifa zinazohodhiwa na serikali ni pamoja na Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari na Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, 2016 ambazo hutoa haki kwa wananchi kupata taarifa. Sheria hizi hazijagusia suala la Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi

Umuhimu wa Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi

Tanzania iliridhia mpango wa EITI mwaka 2012, sheria ya utekelezaji wa mpango huo ilisainiwa mwaka 2015. Mpango huo una lengo la kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji nchini na unawezesha wadau, hasa watunga sera kufuatilia usimamizi wa sekta ya uziduaji hasa kuhusu mapato na kodi inayolipwa na makampuni yanayofanya shughuli za uziduaji. Tangu utekelezaji wa EITI, Tanzania bado haijaweza kutimiza lengo la Uwazi wa Mikataba wala Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi.

Serikali iliyo wazi na yenye kuwajibika huwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa utoaji maamuzi na kutoa mchango chanya katika mapato yanayozalishwa. Hili linawezekana kufaulu pale tu mipango ya uwekezaji ya serikali itaendeshwa kwa uwazi na wananchi na wadau husika kuweza kuchunguza kwa umakini.

Matakwa ya umma ni kuelewa jinsi rasilimali zao zinavyogawanywa na kutumiwa. Ni muhimu wananchi kupashwa taarifa kuhusu utayarishaji wa mikataba ya umma; muundo wa uendeshaji shughuli, mapato, tathmini ya matokeo kwa mazingira, mgawanyo wa mapato, na ushiriki wa wananchi.  Kwa sababu hii, Uwazi, Uingiaji, Usimamizi na Upatikanaji wa Mikataba na Taarifa katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi ni hatua muhimu kwa serikali iliyo wazi.