Siku chache zilizopita, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli aliunda kamati mbili za wataalamu kwa ajili ya kuchunguza taarifa za kuwapo kwa udanganyifu wa kiwango cha madini katika mchanga wa dhahabu (makinikia), ambao umekuwa ukisafirishwa kupelekwa nje ya nchi. Mchanga huo ni ule unaotoka katika migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi ambayo kwa pamoja inamilikiwa na Kampuni ya Acacia.
Kamati hizo pia zilipewa kazi ya kutoa mapendekezo kuhusu namna bora ya kusimamia sekta ndogo ya madini ya dhahabu. Zaidi ya hapo, kamati hizo pia zilitakiwa kuchunguza na kuchambua masuala ya fedha katika shughuli za uchimbaji wa madini nchini. Matokeo ya uchunguzi wa kamati hizo, yalizaa kikao baina ya Rais Magufuli na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick (ambao ni wamiliki wa sehemu kubwa ya Acacia), Profesa John P. Thornton, hatua ambayo imefungua milango ya majadiliano baina ya wawekezaji hao na serikali ya Tanzania.
Baada ya kufuatilia kwa umakini mkubwa matukio haya pamoja na mwitikio wa jamii kuhusu hatua zilizochukuliwa, Jukwaa la Asasi za Kiraia la HakiRasilimali – PWYP tunaofanya kazi ya utetezi katika sekta ya madini, yenye wanachama tajwa hapo chini tunapenda kueleza msimamo wetu.
Tumefanya mapitio ya mihtasari ya taarifa zote mbili tunaunga mkono baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na kamati ambayo yanajenga msingi wa hoja zilizokuwapo tangu mwanzo, hivyo tutapenda kueleza mtazamo wetu kama ifuatavyo:
TUNAMPONGEZA Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake, uthubutu na msimamo wa kuuhisha mjadala wa kitaifa kuhusu usimamizi wa rasilimali za nchi na manufaa yake kwa umma pamoja na dhamira aliyoonyesha ya kuanisha mchakato wa mapitio ya sheria zote zinazosimamia sekta ya madini.
TUNASISITIZA kuwa wananchi wanayo haki ya msingi ya kupata ufafanuzi na maelezo kutoka kwa waliopewa dhamana na wajibu wa kusimamia rasilimali za nchi. Haki hii ni wajibu wa kijamii hivyo kinyume chake ni wahusika kutakiwa kutetea uamuzi waliowahi kuufanya katika mfumo mzima wa uvunaji wa madini dhidi ya thamani halisi ya rasilimali husika. Suala hili linapaswa kwenda sambamba na hatua ya kuwekwa bayana kwa mikataba yote ya uchimbaji wa madini ambayo inapaswa kuwa wazi kwa umma kupitia tovuti ya Wizara ya Nishati na Madini. Ikiwa tunataka kuondoa mashaka na kukosolewa kwa mikaba katika siku zijazo, lazima usiri katika masuala haya ukome kwani unazidisha hali ya wananchi kutowaamini viogozi wenye dhamana ya kusimamia rasilimali hizi.
TUNATAMBUA kwamba uamuzi wa uziduaji wa rasilimali hufanywa kwa kuzingatia mawanda mapana yakiwamo masuala ya kibiashara, huku manufaa yakitarajiwa kupatikana baada ya muda mrefu. Hata hivyo uamuzi wenye sura ya aina hii unaweza kuaminika, kuelewekana kuwa wa maana, ikiwa wananchi wanafahamu mantiki yake kiuchumi na matarajio ya uwekezaji husika, hivyo kuepusha hatari ya kuwapo kwa mkanganyiko wa fikra miongoni mwao.
TUNATOA WITO wa kufanyika kwa mageuzi yenye tija na ufanisi katika mifumo ya sheria, udhibiti wa fedha na usimamizi wa sekta ya madini kwa kuzingatia mambo yafuatayo;
Kuwepo kwa mpango thabiti na huru wa Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za nchi (TEITA), ambao unashirikisha wadau mbalimbali, pia kutambuliwa na kuheshimiwa kwa Asasi za Kiraia (CSO) ambazo watendaji wake wana mchango mkubwa katika kukuza uelewa wa umma kuhusu mapato ya serikali yatokanayo na sekta ya madini pamoja na uhalisia wa kufikiwa kwa matarajio.
Kuhusu wito wa Rais wa kupitiwa upya kwa sheria za madini, tunapenda kutoa hadhari kwamba marekebisho ya sheria zilizopo yasifanywe kwa ‘dharura’ (ikizingatiwa kuwa udharura ambao ulianza kutumika tangu 2010 wakati wa utunzi wa Sheria ya Madini, umesababisha kupitishwa kwa sheria kadhaa pasipo kulipa Bunge na wananchi fursa ya kufanya uhakiki na kujiridhisha kuhusu ubora wake).
Katika mazingira ya sasa kuna kila sababu kuongeza uwazi katika kusaini au kuingia mikataba ya uvunaji / uziduaji wa rasilimali, siyo tu kwa umma bali ushiriki kamilifu wa Bunge katika mchakato huo. Kwa maana hiyo, sheria lazima zitoe fursa kwa Bunge kuisoma na kuijadili mikataba ijayo baada ya kuwa imepita katika hatua za rasimu na majadiliano katika ngazi ya serikali. Hatua hii itasaidia kupunguza uwezekano kutumika kwa udhaifu wowote unaoweza kuwapo katika mfumo wa serikali wakati wa kuingia katika mikataba hiyo ya madini. Uidhinishaji wa mikataba unaoweza kufanywa na wizara, idara na wakala wa serikali (MDAs) pamoja na makubaliano husika kupitiwa na Bunge ni uthibitisho kwamba wawakilishi wa wananchi wanakuwa wamepata muda wa kutosha wa kujadili uhalali wa mikataba kabla ya kuanza kutekelezwa. Pia ni njia mojawapo ya kuyafanya makubaliano husika kuwa chini ya miliki ya umma.
Uhamishaji fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia uuzaji na uagizaji bidhaa nje ya nchi (transfer mispricing) ni suala linaloingilia na kuathiri sera za kodi, ikizingatiwa kuwa linawiana na ushindani wa malengo ya pande tatu katika mfumo wa ulipaji na utozaji wa kodi: kwanza ni lengo la kuongeza mapato kwa mamlaka ya kodi ya ndani, pili ni lengo la kuongeza mapato kwa mamlaka ya kodi ya nje na tatu ni lengo la kupunguza kodi kwa mlipakodi. Kwa maana hiyo, tunaishauri serikali ichunguze ili kubaini iwapo kulikuwa na mchezo wa uhamishaji fedha (transfer mispricing) miongoni mwa kamuni za Barrick, Acacia na kampuni zake zote tanzu. Na ikiwa itabainika kuwapo kwa ‘mchezo’ unaohusisha kampuni hiyo, basi fedha zilizotoroshwa nje zirejeshwe kwa kampuni za Barrick na Acacia kutakiwa kulipa.
HakiRasilimali – PWYP tunaamini kwamba usimamizi wa rasilimali za nchi siyo tu kukusanya mapato, bali pia lazima tuwe na mtazamo mpana wa kuona umuhimu wa kuziongezea thamani rasilimali hizo. Mfumo mzima wa uongezaji wa thamani ya madini unaweza kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi na kukuza ajira. Hata hivyo hayo yanawezekana ikiwa mambo hayo yatazingatiwa katika maboresho yanayokusudia kufanywa. Kwa maana hiyo, tunaukaribisha uamuzi wa serikali wa kujenga kiwanda cha uchenjuaji wa madini ambacho kitakuwa na manufaa ya kiuchumi na kusitisha usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makinikia) kwenda nje ya nchi.
Pamoja na kwamba uamuzi muhimu uliofanywa na Rais umechelewa, unajenga msingi wa kuwa na majadiliano yenye tija kuhusu sekta ya madini katika siku zijazo. Katika kutekeleza maazimio ya timu za wataalamu, HakiRasilimali – PWYP tunaishauri serikali urges governments to be kuzingatia mambo yafuatayo ambayo yanaweza kuwa na matatizo ya kisheria siku zijazo:
Wajibu wa kimataifa wa kisheria ambao serikali imejifunga kuusimamia, kama vile kuzihakikishia kampuni za uwekezaji kwamba mali zao zitakuwa salama na hakutakuwa na utaifishaji;
Umuhimu wa kuendelea kuwa nchi rafiki kwa uwekezaji katika mazingira ambayo yanazinufaisha pande mbili; mwekezaji na serikali; na
Umuhimu wa kuwapo kwa uwazi wa mashauriano wakati wa mchakato wa kubadili mifumo ya sasa ya kisheria na masuala ya fedha katika sekta ya madini.
Imeandaliwa na:
Sekretarieti ya HakiRasilimali – PWYP
Muhimu: HakiRasilimali ni jukwaa la Asasi za Kijamii (CSOs) ambazo zimesajiliwa kama kampuni zisizotengeneza faida chini ya Sheria ya Kampuni ya 2002 ambazo zinafanya kazi mahususi kuhusu masuala ya madini, mafuta na gesi nchini Tanzania. HakiRasilimali ni taasisi mshirika wa Publish What You Pay (PWYP), ambayo inaundwa na wanachama ambao ni muungano wa asasi za kiraia katika nchi zaidi ya 40 duniani kote. Lengo la asasi hizo ni kuhimiza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya rasilimali za madini, mafuta na gesi.
(Wanachama: Action for Democracy and Local Governance, Governance Links, Governance and Economic Policy Centre, Interfaith Standing committee, ONGEA, HakiMadini, Policy Forum, Tanganyika Law Society).