Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Waandaaji wa Kongamano la TAEI (INDABA) 2016,

Watoa mada waliokaribishwa kutoka maeneo mbalimbali Afrika,

Makundi ya madhehebu,

Wawakilishi wa Mashirika ya vyama vya Kijamii,

Wataalamu,  

Washirika wa kimaendeleo,

Wageni waalikwa,  

Mabibi na mabwana,

Habari za asubuhi?

Nichukue nafasi hii kushukuru kwa kupewa heshima hii kuu ya kualikwa kufungua mkutano huu wa (Kongamano-Tanzania Alternative Extractive Industry Conference 2016. Napenda nieleze shukurani zangu kwa Hakirasilimali kwa kuinua heshima ya Indaba katika tasnia hii ya uziduaji.

Nimefurahishwa sana na uwepo wa waalikwa kutoka Nyanja mbalimbali na mashirika yaliyowakilishwa yakiwamo ya mitandao ya kijamii, makundi ya madhehebu ya imani mbalimbali, watafiti, wasomi, washirika wa maendeleo na viongozi wa mashirika ya kiserikali. Serikali inathamini kujitoa kwenu katika mazungumzo haya ambayo yanalenga kujadili tasnia ya uziduaji hapa Tanzania.

Nichukua nafasi hii ya pekee kuwakaribisha washiriki hasa kutoka nje ya Tanzania. Nimejulishwa kuwa tunao washiriki kutoka zaidi ya nchi tano za ki-Afrika na kwingineko (Kenya,South Africa, Uganda, South Sudan, Msumbiji, na Zambia. Kwa ninyi wote tunasema Karibu Tanzania. Ninaamini kuwa mbali na majadiliano ya kusisimua katika mazungumzo yatakayofanyika hapa, mtaweza kupata wasaa wa kufurahia ukarimu wa jiji letu la Dar es Salaam ambalo ndio kitovu cha kibiashsra hapa nchini.

Waheshimiwa mabibi na mabwana,

Katika Afrika yetu hii ya leo, kuibuka tasnia ya uziduaji kumeonyesha kuwa kuna fursa nyingi za kiuchumi ambazo bara hili linaweza kuzitumia kusonga mbele katika matarajio ya kiuchumi na kutoa mchango mkubwa kwenye haki ya kijamii ambamo maendeleo ya pamoja yanaweza kupatikana. Hata hivyo, utandawazi na kuanguka kwa bei ya madini mbalimbali yanayozalishwa hapa nchini na nchi za Afrika na duniani kote hivi sasa na changamoto za kimuundo vinaweka vikwazo kufikiwa maono haya. Ni bahati mbaya kwamba katika baaadhi ya sehemu za Bara la Afrika rasilimali hizi zimekuwa kichocheo na zimezidi kuchochea migogoro baina ya wananchi wenyewe ndani ya nchi za Ki-Afrika na zimeonekana kama laana. Wakati azma yetu ya kufikia malengo 17 ya maendeleo endelevu hadi kufikia mwaka 2030 inabaki pale pale, tasnia ya uziduaji pamoja na chanagamoto zake bado inatoa mwelekeo wa kufikiwa kwa jitihada hizi.

Hatuna budi kuhamasisha juhudi za kuchunguza fursa na changamoto zilizopo ili kuifanya sekta ya uchimbaji iwe kichocheo na iweze kusukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Tangu miaka ya 1990, Tanzania tumejifunza maswala, mifumo na michakato ambamo viwanda vya uchimbaji huibuka, kukua na kuchangia kwenye shughuli za  maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Wakati huohuo matarajio ya kujikomboa kiuchumi kutoka wananchi wetu na jamii yetu yamekuwa juu sana. Ninayo furaha kusema kuwa kujifunza kwetu kupitia wadau mbalimbali wa sekta ya uziduaji, mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali, makundi ya madhehebu mbalimbali na wanoa mbongo kumetusaidia kutuonyesha mbinu mbalimbali tunazoweza kuzitumia.

Tulianza na uchimbaji madini na baadaye tukapanua na kuongeza mafuta na gesi kadri rasilimali zilivyovumbuliwa. Tumeweza kuweka sera na sheria za kusimamia haya pamoja na Sera ya Taifa ya madini na Sheria ya Madini ya 2010. Pia tumejiunga na mpango wa uwazi katika tasnia ya uziduaji duniani (EITI) tangia Mwaka 2009 na kuanzisha kundi la wadau wa sekta ya uziduaji (MSG) ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya kusimamia masuala ya uzidua nchini ya Mwaka 2015. Hatua hizo pamoja na zingine muhimu katika kuhakikisha kuwa rasilimali zetu ambazo mungu ametujalia zinatunufaisha watanzania wote na kuziba mianya ya watu wachache kujinufaisha wenyewe nakuacha wengine wanakuwa watazamaji.

Hapa tulipo tunaendelea kufanya mageuzi ya vyombo ili kuhakikisha kuwa taifa linafaidika na rasilimali hizi. Ninaamini nchi zingine pia zimepitia njia kama hii. Hivyo basi hakuna sababu ya kuridhika na kuacha kuunganisha uwezo uliopo katika rasilimali zinazochimbwa.

Nimeambiwa kuwa mkutano huu wa siku mbili utajadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na haki za kijamii, sera za tasnia ya uziduaji, uchimbaji mdogo, mapato na mtiririko wa fedha haramu.

Yawezekana siku hizi mbili zinaweza zisitoshe kujifunza, kuibua sauti kutoka kwenye Nyanja mbalimbali na kupeana uzoefu, lakini pia ninaamini kuwa wote tutafaidika kutokana na mawazo mbalimbali na mapendekezo yanayotokana na ushahidi kutoka kwa washiriki mwishoni mwa kongamano hili.

Mandhari ya kongamano hili, ‘’Bila Kumwacha mtu nyuma: Kufanya rasilimali ziwanufaishe watu’’ inaonyesha hamu ya kuchangia kwa watu wengi zaidi kupitia usimamizi wa kina wa rasilimali, hasa katika sekta ya uchimbaji. Hii ni kazi muhimu sana kwetu katika mkusanyiko huu na wale ambao wangependa kusikia na kujifunza kutokana na mapendekezo ya kongamano hili.

Waheshimiwa mabibi na mabwana,

Kuna maswali mengi sana yanayozunguka kwenye tasnia ya uziduaji hapa Afrika. Kwetu sisi Tanzania, tunaamini kuwa tuendelee kufanya mageuzi ya sera na mazoea ili kuhakikisha kuwa watendaji wote wakiwemo wa Serikali na watu binafsi wanakuza mbinu bora kwaajili ya maadili ya pamoja, uraia mwema, masuala mema ya kijamii na kimazingira, usimamizi wa jamii pamoja na kuchunguza kwa makini mikakati endelevu. Kupitia majadiliano haya, ninaamini tunaweza kupata michango ya kufaa kwaajili ya mchanganyiko wa sera na kanuni.

Waheshimiwa mabibi na mabwana,

Kwa upande wetu, napenda kuwahahakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na makundi mbalimbali katika kazi ya kupata matukio ya kufaa kwaajili ya usimamizi wa tasnia ya uziduaji nchini.

Napenda tena kushukuru HakiRasilimali, na uwepo wa makundi ya Madhehebu, mitandao ya kiraia na wanoa bongo kwa kunikaribisha kushiriki mwanzoni kabisa mwa mazungumzo haya. Ahsanteni sana.

Tunataraji kongamano lenye msisimko na la kujenga na kuwatakia wote ushiriki wa kujenga.

Kwa maelezo haya mafupi, sasa ninatamka kuwa mkutano huu wa kimataifa, Indaba 2016, hapa Dar es Salaam umefunguliwa rasmi.