Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

ASASI ZA KIRAIA KUITISHA MKUTANO WA KITAIFA WA TASNIA YA UZIDUAJI

Ufanisi na matumizi bora ya maliasili kwa manufaa ya umma

Umoja wa Wadau wa HakiRasilimali kwa kushirikiana na wanachama wake: HakiMadini, Interfaith Standing Committee, Policy Forum, ONGEA na Governance Humbly Links wameandaa mkutano wa kitaifa wa tasnia ya uziduaji utakaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl Ubungo, Dar es Salaam tarehe 26 na 27 Oktoba, 2016.  Mkutano utaanza saa 8:00 asubuhi.

Lengo la mkutano ni kubadilishana mawazo na uzoefu ili kuimarisha uelewa wa makundi mbalimbali kuhusiana na tasnia ya uziduaji. Pia kutakuwa na mjadala kuhusu jinsi tasnia ya uziduaji inavyoweza kuchangia kuinua uchumi wa nchi.

Mkutano huo unalenga hasa kusisitiza matumizi bora ya maliasili kwa manufaa ya umma.

Malengo ya mkutano ni:

I. Kutathimi kwa kina namna ya upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya shughuli za uziduaji na madhara yake kwa jamii

II. Kuelezea  umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika tasnia ya uziduaji

III. Kutathmini uhusiano kati ya uwajibikaji na maendeleo ya uchumi kupitia tasnia ya uziduaji

IV. Kupitia upya sera zinazohusu wachimbaji wa kati na wadogo wa madini

V. Kuchochea ushirikiano na kujenga muungano baina ya asasi za kiraia, jamii na wachimbaji wa kati na wadogo.

Mikutano ya kitaifa ya tasnia ya uziduaji ilianza mwaka 2011 ambapo Wadau wa Umoja wa HakiRasilimali na asasi nyingine za kiraia waliungana na Wizara ya Nishati na Madini na kuandaa mkutano uliofanyika Jijini Arusha.

Mwaka 2012, Wadau wa Umoja wa HakiRasilimali  waliandaa mkutano wa kwanza wa kipeke uliolenga jamii na wachimbaji wa kati na wadogo walioathiriwa na shughuli za uziduaji.

Washiriki wa mkutano wa mwaka 2016 ni mashirika ya kiraia, mashirika ya dini, wawakilishi kutoka jumuiya za wachimbaji, vyombo vya habari, mashirika ya maendeleo, makampuni ya madini, wachimbaji wa kati na wadogo kutoka Tanzania, Kenya na Uganda, mwakilishi wa serikali, na makundi mbalimbali ya kijamii kutoka Afrika Kusini, Zimbabwe, Uganda na Kenya.

Kwa taarifa zaidi, wasiliana na Racheal Chagonja kupitia barua pepe coordinator@hakirasilimali.or.tz au namba ya simu 0745 655 655

_____________________

Racheal Chagonja

Mratibu HakiRasilimali