Tarehe 16 Juni 2015 Serikali ya Tanzania ilipeleka miswada mitatu bungeni inayohusu sekta ya uziduaji chini ya “Hati ya Dharura.” Miswada hiyo ni Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2015 (The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act 2015, Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015. (The Oil and Gas Revenue Management Act 2015) Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 (The Petroleum Act 2015).
Kwa msingi huu, sisi wana Asasi za Kiraia (AZAKI) kwa majina tajwa hapa chini tulikutana na kujadili miswada hiyo jijini Dares Salaam kuanzia tarehe 21 hadi 23 Juni, 2015 kwa lengo la huchambua na kuboresha miswada ya sheria zilizopendekezwa kwa manufaa na maslahi mapana ya taifa .
TUNAIPONGEZA sana Serikali kwa juhudi zake katika kusimamia rasilimali hizi za taifa kimkakati kwa madhumuni ya kuleta ufanisi na kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo hapa nchini.
TUNASISITIZA ukweli kwamba, kwa ujumla, miswada yote mitatu ina vifungu vingi vyenye kulinda maslahi mapana ya taifa pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta na kuhakikisha uwazi na kuendeleza uchumi imara.
Pamoja na hayo, tuna WASIWASI na hofu kubwa juu ya wakati na haraka iliyotumika katika kuandaa na kuwasilisha Bungeni miswada hii muhimu ya sheria., ikizingatiwa kwamba imekuwa ni ada na kawaida ya serikali kuwasilisha bungeni miswada muhimu tena kwa hati za darura kama ilivyokuwa mwaka 2010 kwa Sheria ya Madini. Muhimu zaidi, ni kuhakikisha kuwa Serikali inaweka sheria zilizo sahihi.katika usimamizi wa sekta husika.
TUNAWASIHI Wabunge kupitia miswada hii kwa uangalifu japokuwa tunafahamu kuwa nguvu kubwa na mitazamo ya wabunge walio wengi kwa sasa emeelekezwa zaidi kwenye uchaguzi mkuu ujao na huenda ikasababisha vipaumbele na umakini katika kujadili miswada hii kupungua kwa kiasi kikubwa kama tulivyo shuhudia mahudhuriio hafifu bungeni katika mkutano wa bajeti unaoendelea
Rasimu ya Sheria ya Petroli ya mwaka, 2015
Wakati muswada unaweka muundo wa kitaasisi- ili kusimamia sekta ya petroli, unalenga kuimarisha udhibiti na weledi katika kuendesha sekta, hata hivyo kuna vifungu vinavyo sababisha kuingiliana kiutawala, Vifungu hivi kama vitapitishwa bila kurekebishwa, chuenda vikaathiri motisha na kuleta msuguano kati ya taasisi zinazopendekezwa kuanzishwa katika muswada huu. hivyo kuhatarisha usimamizi madhubuti wa sekta ya petroli.
Matumizi neno “pekee” (exclusive) juu ya mamlaka ya Kampuni ya Taifa ya Mafuta (National Oil Company) katika vifungu 10 (2) na 45 inaweza kuleta utata katika tafsiri na kuleta changamoto kiuwajibikaji. Wakati mfumo kama huu unaweza kuwa na faida fulani katika kujenga uwezo wa kampuni hiyo kujifunza biashara na kujipangia mikakati yake ya ubia bila vikwazo, kuna hatari kuwa uchaguzi wa wabia utategemea zaidi faida za kiuchumi za kampuni ya taifa ya mafuta(NOC) kuliko maslahi mapana ya taifa kwa ujumla. Hii ni kinyume na madhumuni ya Sera ya Taifa ya Gesi na rasimu ya Sera ya Petroli.
Kifungu cha 6:“Kamishna wa petroli atakuwa mshauri wa Waziri kuhusu sera, mipango na kanuni pamoja na masuala ya utawala ya siku hadi siku katika sekta ya petroli na sekta ndogo ya gesi.”
Wasiwasi / Mashaka: Kuunda nafasi ya kamishna wa petroli ambaye atakuwa katika nafasi sawa na kamishna wa nishati kunaweza kuleta muingiliano/mgongano katika majukumu, lakini kisera na kitaalamu petroli kama bidhaa iko chini ya sekta ya Nishati.
Tunapendekeza: Kuunda nafasi za Naibu Kamishna wa nishati anayeshugulikia maswala ya Petroli akiwa na wajibu /majukumu mahususi ya kusimamia sekta ya Petroli na/au Nishati kwani kuna umuhimu wakuimarisha ofisi ya Kamishna wa Nishati kwajili ya kuondoa muingiliano na mgongano wa kiutendaji.
Kifungu 45: “Kampuni yaTaifa ya Mafuta itakuwa na “haki ya pekee” katika uchimbaji wa mafuta chini ya Sehemu hii.”
Wasiwasi: vifungu hivi viwili vinapingana na Kifungu 45 (4) kinachoelezea mgawo/hisa kwa kampuni yaTaifa ya Mafuta (NOC) na kifungu 219 (1) ambacho kinaipa serikali uwezo wa kuamua mgawo/hisa hivyo kuibua changamoto za kiuwajibikaji pamoja na urasimu a wa kitaasisi.
Tunapendekeza: Haki ya pekee kwa kampuni ya taifa ya mafuta(NOC)iwekewe sharti la kuidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifungu 101 (3): “ Mwenye leseni na mkandarasi hawatachoma gesi au kucheu na kumwaga mafuta bila ruhusa ya awali toka kwa PURA.”
Tuna wasiwasi; kwamba sheria inayopendekezwa inaifanya PURA kuwa na uamuzi wa mwisho bila kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mamlaka za usimamizi wa mazingira kama Tume ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Tunashauri: Waziri awe na mamlaka ya mwisho ya utoaji kibali cha kuchoma gesi au kucheua mafuta baada ya kupata ushauri wa kimaandishi kutoka PURA na NEMC.
Zaidi ya hayo, ni muhimu sana kwamba muswada huu kuweka vipengele vinavyolazimisha uchapishaji wa taarifa muhimu ili kuongeza uwazi wa sekta ya mafutana gesi. Taarifa hizi zijumuishe: Taratibu za utoaji zabuni ikiwemovigezo vya kushiriki na kushinda zabuni hizo, orodha ya makampuni yanayoweza kushiriki, vigezo vya kupata mshindi , orodha ya washindani, washindi wa zabuni, taarifa ya tathmini ya o wa zabuni ikithibitisha ushindi ulivyopatikana na vigezo vilivyotumika. Pia taarifa ya Mikataba yenye maelezo yote, pamoja na marekebisho na viambatanisho vyake, na mnufaikaji kutokana na umiliki wa leseni (beneficial ownership of license holders), matokeo ya tathmini ya kimazingira, mipango ya usimamizi wa mazingira, na taarifa za mwaka na mipango ya kuendeleza unufaikaji kwa wananchi
1.1 Muswada wa Sheria yaUsimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015
Muswada wa Sheria inayopendekezwa una vipengele muhimu sana kuhakikisha usimamizi makini wa mapato yanayotokana nauchimbaji wa mafuta na gesi; kuendeleza uimara wa fedha na uchumi mkuu na kupanga mikakati ya uwekezaji sambamba na vipaumbele vya mipango ya maendeleo ya muda wa kati na muda mrefu, hivyo kuleta maendeleo endelevu. Lakini, kanuni / taratibu za fedha zilizopendekezwa hazihakikishi haki sawa baina ya vizazi kwa maana ya kuweka akiba sehemu ya mapato kwa ajili ya vizazi vijavyo kama ilivyo katika Sera ya Taifa ya Gesi Asilia ya mwaka 2013.
Kuweka ukomo wa utengaji fedha kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa kiwango cha 60% ya fedha zilizohawilishwa kwenye akaunti ya jumla kunaweza kuathiri mahitaji ya uwekezaji kama huo wakati uwezo wa kutumia utakaporuhusu matumizi ya hadi100% au zaidi ya fedha zilizohawilishwa kwenye akaunti ya jumla/pamoja kutoka kwenye mfuko. Zaidi ya hayo, sheria iliyopendekezwa haielezi waziwazi kuhusu marekebisho ya mapungufu ya fedha (Kifungu 17. (1)(b). Kwa uelewa mzuri zaidi, kifungu hicho kinapaswa kuboreshwa zaidi kuhakikisha kuwa marekebisho ya mapungufu ya fedha yanatilia maanani muda wa mzunguko wa mapato (ukiondoa mapato yaliyodhihirika ya mafuta na gesi ) kutoka muda huo ambapo mapato yanafikia walau kiwango kilichopangwa cha 3% ya GDP (Zao Ghafi la Ndani / Pato la Taifa) wakati mapato yanaposhuka moja kwa moja chini ya kiwango kilichopangwa.
Wakati sheria iliyopendekezwa ina lengo la kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa uwekezaji wa Kampuni yaTaifa ya Mafuta (NOC , kufunga fedha za NOC kwa kiwango cha 0.1% za GDP hakutoi uhakikisho wa mgawo wa mapato unaofaa kwa kuzingatia malengo yake na/au uwezo wake wa kimatumizi. Ili kuondokana na uwezekano wa changamoto ya ama kutoa fedha kidogo au zaidi kwa NOC, serikali inaweza kufikiria kutoa fedha kwa kupitia Akaunti ya Jumla/Pamoja (Consolidated Account) kwa kutegemea mipango ya uwekezaji ya NOC ya muda wa kati na ya muda mrefu.
1.2 Sheria ya Tasnia vya Uziduaji (Uwazi na Uwajibikaji) ya Mwaka 2015
Tunaamini kuwa sheria iliyopendekezwa itaimarisha maazimio ya Tanzania ya kuongeza uwazi wa mapato yaliyoanza kwa kujiunga na EITI (Global Movement) mwaka 2009. Tunaona kuwa tangu hapo kikundi tekelezi cha TEITI kimeendeshwa kwa kutumia hati za Makubaliano (Memorandum of Understanding), bila kuwepo kwa sheria zozote. Sheria inayopendekezwa itatoa msingi wa kisheria kwa kuhakikisha utekelezaji wa maazimio kama inavyoelekezwa kwa viwango vya EITI kimataifa sambamba na maazimio ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuimarisha uwazi katika uendeshaji wa shughuli zake.
Lakini kuna mapungufu ya wazi katika sheria hii iliyopendekezwa ikiwemo kuifanya kikundi tekelezi kuwa chombo au sehemu ya taasisi za kiserikali hali itakayoikosesha uhuru. Tunaomba serikali ihakikishe kuwa chombo cha usimamizi (TEITI MSG) kinapewa uhuru katika kuchagua wajumbe wake, kutafuta rasilimali watu na fedha ili kuilinda dhidi ya kuingiliwa kisiasa..
Pamoja na hayo, viwango vya chini vya adhabu vilivyopendekezwa katika rasimu hii kwa watakaokosa kutoa taarifa haviakisi thamani ya tasnia ya uziduaji na inahitaji mapitio.
Imetiwa Sahihi na :
- Governance Links
- Policy Forum
- Oil, Natural Gas & Environmental Alliance (ONGEA)
- HakiMadini
- Interfaith Standing Committee on Economic Justice
- Governance and Economic Policy Center
- International Alliance of Natural Resources in Africa (IANRA)