Kufuatia ugunduzi wa uhakika wa hivi karibuni wa gesi asilia Tanzania, nchi imejitokeza kuwa na uwezekano mkubwa wa uzalishaji gesi kwa kiwango cha juu katika Afrika ya Mashariki, na kuleta hamasa miongoni mwa wananchi, jumuiya za kiraia, na wanasiasa kuhusu matarajio ya rasilimali hiyo kuchochea maendeleo ya taifa . Serikali, inaaminika, imeanza mchakato wa kuandaa sera na miundo ya kisheria zitakazosaidia usimamizi wa uchunguzi, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia. Kumekuwa na malalamishi mengi hata hivyo, kwamba siyo mengi yalifanyika kuboresha uwazi katika sera za kifedha na masharti ya mikataba ya uziduaji kwa ujumla.
Taarifa za kuvuja hivi karibuni kwa Mkataba wa Nyongeza wa Ushirikiano katika Uzalishaji (Production Sharing Agreement -PSA) kati ya “Statoil”, yaani Kampuni ya Mafuta ya Taifa la Norway na Serikali, na utata uliozuka miongoni mwa wananchi, zinaonesha umuhimu wa utaratibu wa kuweka wazi mikataba yote inayohusu uziduaji nchini Tanzania.
Sisi Asasi za Kiraia tajwa hapa chini, tumekuwa tukifuatilia majadiliano na maoni ya wadau mbali mbali kuhusu suala hili kwa shauku kubwa. Kama matokeo yake, tarehe 15th ya mwezi wa Agosti, 2014 tulijadili kuhusu chambuzi mbali mbali kwa lengo la kutoa maoni yetu kama asasi za kiraia na msimamo wetu kuhusu hali ya utata iliyojitokeza kufuatia uvujaji wa Mkataba wa Nyongeza wa Statoil kwa manufaa ya taifa.
TUNAELEWAkwamba uziduaji wa rasilimali unajumuisha maamuzi magumu yenye mwingiliano mkubwa, makubaliano ya kibiashara yenye maslahi kwa pande zote na masharti ya muda mrefu. Haya maamuzi yatakuwa ya kuaminika zaidi na hayatakiukwa kwa urahisi ikiwa wananchi wanaelewa sababu za kiuchumi zilizofanya maamuzi hayo kuchukuliwa. Jambo la msingi hata hivyo, ni kwamba sera za kifedha na masharti ya mikataba ni budi yazingatie kuwa nchi inanufaika ipasavyo kutokana na rasilimali, pamoja na kuvutia uwekezaji unaohitajika ili kupata manufaa yanayotakiwa. Serikali na wawekezaji kwa kawaida hupata huduma bora zaidi iwapo kuna kanuni / sheria za wazi zinazofuatwa na wawekezaji wote kwa mazingira yanayofanana. Uwazi na sheria / kanuni zinazofanana husaidia kufanya watendaji kufahamu kuwa huduma hazibagui, hupunguza fursa za rushwa na huweza kupunguza madai kutoka kwa wawekezaji mmoja moja kupewa upendeleo fulani .
TUNASISITIZA haki ya uwajibikaji kijamii kwa maana kwamba wananchi wana haki ya msingi kupata maelezo na uthibitisho toka kwa watendaji waliopewa wajibu wa kusimamia mali asili zao. Kwa upande mwingine, watendaji nao wanapaswa kutoa uthibitisho kuhusu maamuzi wanayofanya katika utumiaji wa hizi rasilimali.
TUNASIKITISHWA na ufinyu wa taarifa zinazotolewa kwa umma hali inayopelekea katika uharibifu na hali ya hatari na ya kukanganya kuhusu mikataba ya gesi asilia na viwanda vya uziduaji kwa ujumla. Uvujaji wa taarifa za Mkataba wa Nyongeza wa Ushirikiano katika Uzalishaji (PSA) uliopo kati ya Serikali na Statoil unaibua masuala haya:
· Mwitikio mdogo kutoka kwa Serikali na kutokuwepo mwitikio kabisa kutoka Statoil kunaleta hali ya kutokuwa na uhakika na ya mashaka. Mwitikio wa serikali kwa kupitia tamko kwa vyombo vya habari lililotolewa na TPDC kwa ujumla linadai kuwa masharti ya PSA hiyo ni mazuri kwa nchi kwa kunukuu 61% zinazoingia serikalini. Tamko liliendelea kutuhumu vyombo vya habari kwa kutokuwa na taarifa wakati huo huo likitoa maelezo yasiyo sahihi kwamba bila Statoil kutia sahihi PSA mwaka 2007, ujazo wa futi trilioni 50. 5 usigegundulika, kwa hiyo kudhania kuwa ugunduzi wote unatokana na Statoil! Hili linaibua swali zaidi kama tofauti iliyopo ni malipo ya ziada (bonasi) kwa Statoil kwa ajili hiyo? Tamko halitoi taarifa zozote kuhusu sababu za msingi za kiuchumi na matarajio yaliyotegemewa kuthibitisha tofauti kutoka Mkataba wa Nyongeza wa Mfano na PSA wala masharti halisi ya mkataba wa PSA uliotiwa sahihi.
· Ukimya mkubwa wa Statoil kuhusu suala ambalo linatishia siyo tu sifa yake kama kampuni bali na ya nchi yake (Norway) iliyo mstari wa mbele katika uwazi wa viwanda vya uziduaji.
· Mmomonyoko unaoendelea wa imani ya umma kuhusu jinsi sekta ya uziduaji inavyosimamiwa kwa kuchota uzoefu unaotisha wa sekta ya uchimbaji madini. Ikiwa umma utaaminishwa kuwa mkataba wa serikali na Statoil ulikuwa mzuri kutegemea taarifa walizokuwa nazo wakati wa kutiliana sahihi kwenye Mkataba wa Nyongeza, taarifa zote husika lazima ziwekwe wazi.
· Usiri unaoendelea kuhusu suala hili ambalo sasa hivi linajadiliwa na umma unaongezea hali ya wananchi kutokuwaamini hao waliopewa jukumu la kusimamia rasilimali. Uchambuzi wa hivi karibuni wa Taasisi ya Usimamizi wa Mali Asili (The Natural Resource Governance Institute - NRGI) unaonyesha kuwa inawezekana kuwa ni mapema mno kuwa na uhakika kama Tanzania ilipata au haikupata kiwango kikubwa kutokana na Mkataba wa Nyongeza wa Statoil wa mwaka 2012 kwa kuzingatia kuwa Mkataba wa awali wa PSA wa mwaka 2007 na taarifa nyingine zilizowezesha mahesabu ya serikali bado hazipatikani kwa umma.
· Namna ambavyo Mkataba wa Nyongeza wa Statoil uliletwa na kuanza kujadiliwa na umma (kwa kuvuja) inashusha hadhi ya serikali kwani inaleta mashaka mengi na inaweza kufanya wengine kudhani kuwa lengo lilikuwa kufichua rushwa katika makubaliano hayo. Uvujaji huo unawasukuma wadau wote: viwanda, serikali na jumuiya za kiraia kuanza mazungumzo ya dhati kuhusu usiri unaoendelea katika mikataba ya viwanda vya uziduaji ingawa manufaa ya kuweka mambo wazi yanaonekana waziwazi.
· Kuzuia suala muhimu la umma kujadiliwa kwa taarifa nusunusu za kuvuja, wadau sharti waanze majadiliano ya kweli na ya wazi kuhusu uhalali wa kisheria wa serikali na viwanda vya uziduaji kukataa mara nyingi kuweka wazi mikataba hiyo.
· Ieleweke pia kuwa uwazi wa mikataba ni sharti moja kwa makampuni (e.g. mfano Swala kupitia sharia za Mamlaka ya Masoko ya Dhamana na Mitaji) na itakuwa lazima kwa mikataba ya uziduaji itayotiwa sahihi baada ya 2014 kama serikali ijayo itadumisha dhamira chini ya Mpango Kazi wa Mpango wa Uendeshaji Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership Action Plan). Tunauliza kwa nini kampuni zingine zishinikizwe kuwa wazi wakati zingine hazilazimishwi?
· Jumuiya za kiraia, wabunge na wananchi wamekuwa wakitoa hoja za kutaka bunge lipitishe mikataba ya uziduaji baada ya rasimu za mikataba hiyo kuandaliwa na kujadiliwa na serikali. Upitishwaji wa Mkataba wa Statoil (PSA), Mkataba wa Nyongeza na Mikataba mingine kama hiyo na Bunge kungehakikisha kuwa wawakilishi wa wananchi wamepata muda wa kutosha kujadili ubora wa mikataba hiyo kabla haijaanza kutekelezwa na ni njia nyingine ya kuleta mikataba hiyo mbele ya umma. Pia inazuia makampuni kuhamisha rasilimali kwenda nje ya nchi kimagendo. Serikali inaweza kusita kuhusu mkataba wa Statoil kuwekwa wazi kwa umma kwa maana kutaweza kuthibitisha kwa umma kuwa Mkataba wa Nyongeza wa Statoil PSA ulikuwa kweli hauna maslahi mazuri na hivyo kuibua madai ya kuujadili mkataba huo upya (renegotiation). Hili siyo lazima liwe na madhara kwa serikali wala kwa makampuni. Kutokana na mabadiliko katika hali ya kiuchumi, ni kawaida kwa mikataba ya uziduaji kujadiliwa upya bila kuvuja kwake. Kuingia mkataba mpya kunaweza kusaidia kurudisha imani kwa wananchi na kusaidia shughuli za uziduaji kufanyika kwa tija kwa mtazamo wa muda mrefu.
· Mjadala mrefu wa umma kuhusu Mkataba wa Nyongeza wa Statoil (PSA) unaonesha uelewa tofauti juu ya mikataba ya uziduaji. Uelewa mdogo wa nini kiko ndani ya mikataba hii unazuia juhudi za kuweka uwazi katika sekta ya uziduaji.
Kutokana na yaliyotajwa hapo juu, TUNATAKA Serikali:
· Iweke wazi kwa umma Mkataba uliotiwa sahihi (nakala halisi) wa Statoil (PSA) wa mwaka 2007 kwa uchambuzi wa umma.
· Iweke wazi kwa umma mikataba yote 25 ( PSAs) iliyowekwa sahihi pamoja na mipya itakayotiwa sahihi kwa lengo la kutoa haki sawa kwa wadau wote katika viwanda.
· Ianzishe utaratibu wa bunge kuridhia mikataba yote ya uziduaji baada ya kujadiliwa na kutiwa sahihi na Waziri husika.
· Jamii, vyombo vya habari na serikali budi zitoe kipaumbele katika kuhakikisha kuwa uwezo wa wadau wao kuingia katika mijadala ya uziduaji unaimarishwa
Zaidi ya hayo,TUNATAKA:
· Statoil itoe maelezo kwa umma kuhusu sababu zilizowasukuma (kama zipo) za kutenda tofauti na Mkataba wa Mfano (Model PSA)
· Makampuni yote ya Mafuta, Gesi na uchimbaji madini yanayoendesha shughuli zao Tanzania na serikali kufanyia mapitio vipengele vyote vya usiri katika mikataba ya uziduaji kwa manufaa ya umma na yaache kuingiza vipengele kama hivyo katika mikataba mipya.
TUNAPENDEKEZA yafuatayo ili kufanyia kazi suala zima la usimamizi wa uziduaji:
· Kuunda Sheria ya Uhuru wa Habari
· Kuanzisha hifadhi ya mikataba kwa kutumia kompyuta (database)
· Makampuni ya Uziduaji yafanyie mapitio sera zao za usiri.
Wadau:
1. Interfaith Standing Committee on Economic Justice and the Integrity of Creation
2. HakiMadini
3. Policy Forum
4. Oil and Natural Gas Environment Alliance (ONGEA)