Skip to main content

Policy Forum (PF) ni mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) ambao ulianzishwa mwaka 2003, uliosajiliwa chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali iliyoundwa chini ya Kifungu cha 11 (1) na 17 (2) cha Sheria Na. 24 ya 2002. Uwanachama wetu kwa sasa unajumuisha zaidi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali zaidi ya 60 yaliyosajiliwa Tanzania. Nia yetu ni kuboresha michakato ya sera ili kupunguza umaskini, kuongeza usawa na demokrasia.

Sisi ni mtandao unaoongozwa na wanachama, kwa hiyo chombo chetu cha juu cha kufanya maamuzi ni Mkutano Mkuu unaoundwa na wanachama wote wenye hadhi ya kupiga kura katika mtandao. Shughuli zetu zinasimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi, iliyochaguliwa na wanachama na kutumikia kwa kipindi cha miaka 2. Wajumbe wa Bodi husimamia ofisi ndogo ya Sekretarieti iliyoundwa kuratibu, kuwezesha, kufuatilia na kuripoti shughuli za mtandao.

Mtandao unaoongozwa na wanachama hufanya kazi zaidi kupitia vikundi viwili vya kazi ambavyo ni Kikundi Kazi cha Bajeti (BWG) na Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa (LGWG), kila kikundi kazi huleta pamoja wanachama kushawishi michakato ya bajeti na sera mbalimbali kupitia mijadala ya kimkakati kwa kutumia majukwaa tofauti katika ngazi ya kitaifa na msingi. Mtandao pia unaratibu kikundi kinachofanya kazi cha masuala ya haki za kodi na pia mtandao ulisaidia sana kuundwa kwa asasi inayojishughulisha na uziduaji nchaini, HakiRasilimali.

Bodi ya Wakurugenzi huchaguliwa na wanachama kupitia Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) unaofanyika kila robo ya kwanza ya mwaka. Mtandao unaratibiwa na Sekretarieti yenye wafanyikazi 11 ambao hurahisisha masuala muhimu ya kiutendaji, kiutawala na kifedha.

Dhima

Maisha bora kwa Watanzania

Dhamira

‘Kushawishi michakato ya sera ya kuimarisha uwajibikaji na matumizi yenye kuzingatia usawa ya rasilimali za umma kupitia ubia ulioboreshwa’

Maadili ya Msingi

Maadili ya msingi ya Mpango Mkakati wa Sita yanatokana na Mipango Mikakati iliyopita ambayo imekuwa ni sehemu ya utamaduni wa Policy Forum. Maadili hayo ni kama ifuatavyo;

a. Ushiriki – Policy Forum inaamini katika demokrasia shirikishi na litafanya kazi kukuza nafasi ya kidemokrasia kwa ajili ya sauti na hatua za umma.

b. Uwajibikaji – Policy Forum hufanya kazi kukuza uwazi na uwajibikaji katika mashirika yetu, ubia na katika jamii.

c. Mshikamano – Policy Forum huunda umoja na watu wenye nia zinazoendana na mtandao na mashirika yanayosimimia kwa dhamira yake.

d. Uhuru - Wananchama wa mtandao ni mashirika huru na yasiyo fungamana na upande wowote, yanayosimamia dhamira, maadili bila kushawishiwa maagizo ya serikali yoyote ya ndani, ya kitaifa au ya kigeni.

e. Usawa - Kwa sababu watu wote ni sawa, Policy Forum itaendeleza kikamilifu haki za binadamu, utu, usawa na kujumuishwa kwa watu wote.

f. Uadilifu – Mtadao hufanya kazi kwa kuzingatia viwango vya juu vya uaminifu na kanuni imara za maadili

g. Kujifunza - Mtandao utaendelea kudumisha ubora na utamaduni wa kujifunza na kutafakari

Mabadiliko Yanayotarajiwa

Ubora wa maisha unaotokana na  utumiaji unaozingatia usawa katika matumizi ya rasilimali za umma na uongozi shirikishi.