Skip to main content
Submitted by Web Master on 30 October 2017

HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (OR-TAMISEMI) MHE. SELEMANI JAFO (MB) WAKATI WA UZINDUZI WA MIONGOZO YA MFUMO WA UTOAJI WA RUZUKU YA MAENDELEO YA SERIKALI ZA MITAA (LGDG) MJINI DODOMA, 28 OKTOBA 2017

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma,

Wenyeviti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Bahi,

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma,

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Bahi,

Mwenyekiti wa Bodi ya Policy Forum,

Wakurugenzi wa Idara na Vitengo OR-TAMISEMI,

Mratibu wa Policy Forum,

Wataalamu kutoka Policy Forum na OR-TAMISEMI,

Waandishi wa Habari,

Washiriki wote Mabibi na Mabwana,

Habari za mchana,

Ndugu washiriki,

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa katika tukio hili muhimu la uzinduzi wa Miongozo ya Mfumo wa utoaji wa Ruzuku ya Maendeleo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM).

Ndugu washiriki,

Miongozo ya mfumo wa utoaji wa Ruzuku ya Maendeleo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa inayozinduliwa leo imeandaliwa na OR-TAMISEMI kwa ufadhili na msaada wa kitaalamu wa Shirika la Policy Forum (PF). Naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana wataalamu wa pande hizi mbili kwa kufanya kazi ya kuitafsiri miongozo hii kwa Lugha rahisi ya Kiswahili, lugha ambayo inaeleweka vizuri kwa wananchi wote hasa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao ndio walengwa Wakuu wa Miongozo hii.

Ndugu washiriki,

Mnamo mwaka 2016, OR-TAMISEMI iliomba msaada wa Policy Forum (PF) wa kuandika kwa lugha rahisi ya Kiswahili na usambazaji wa Miongozo hiyo, ambayo itasambazwa na kutumika katika ngazi za Serikali za Mitaa nchini. Kazi hiyo nimeelezwa imekamilika. Nimeetaarifiwa pia kwamba, Policy Forum waligharamia zoezi hilo, pia wameahidi kuisambaza katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, nawapongeza sana kwa kujitolea kwenu na kuonesha ni kwa jinsi gani mpo nasi bega kwa bega katika kuhakikisha tunaimarisha Serikali zetu za Mitaa ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naomba kuwakumbusha tena kuwa, Miongozo ya Mfumo wa utoaji wa Ruzuku ya Maendeleo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa inajumuisha maeneo matatu muhimu ambayo ni:-

  • Mwongozo wa Utekelezaji na Uendeshaji.
  • Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini;
  • Mwongozo wa Upimaji wa Matokeo kwa Mwaka

Ndugu washiriki,

Jumla ya nakala 33,600 tayari zimeshachapishwa na Policy Forum na baada ya uzinduzi huu, zitasambazwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Nitoe wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zote Nchini kuhakikisha kuwa miongozo hii haiwekwi kwenye makabati, bali inatumika kwa malengo iliyokusudiwa ili iweze kuleta ufanisi katika utendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Naambiwa pia, Policy Forum wako tayari kuchapisha na kuzisambaza nakala nyingi zaidi pindi itakapoonekana zilizopo hazitoshelezi mahitaji. Asanteni sana Policy Forum kwa msaada huo.

Ndugu washiriki,

Napenda pia kupongeza uamuzi mliofikia wa kuwa na Mkataba wa ushirikiano baina ya Policy Forum na OR-TAMISEMI wenye lengo la kurasimisha mahusiano yetu na kupanua wigo mpana zaidi wa kuendelea kushirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili. Ni imani yangu kwamba makataba wa ushirikiano unaotarajiwa kusainiwa mapema iwezekanavyo ili azma yetu ya kuimarisha ushirikiano iweze kutimia.

Ndugu washiriki,

Natumia nafasi hii, kwa mara nyingine kuwatakia kila lakheri katika kudumisha ushirikiano wa kitaalamu na naamini huko tuendako tutaendelea kushirikiana zaidi tukiwa na lengo moja la kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa weledi na uadilifu katika ngazi zote za Serikali za Mitaa ili tuweze kuboresha zaidi utendaji wetu na hivyo kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ndugu washiriki,

Kwa maneno hayo machache, natangaza rasmi miongozo ya Mifumo ya utoaji wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa nimeizindua rasmi. Natoa rai kuanzia leo OR-TAMISEMI na Policy Forum muanze kuisambaza miongozo hii katika Halmashauri zote nchini kama mlivyojipanga.

Asanteni sana