Uwajibikaji Jamii Kutatua Changamoto za Sekta ya Afya na Elimu

Categories

Novemba 2020,  wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na Wanachama wa Policy Forum walihudhuria vikao vya tathmini za kikanda za masuala ya Uwajibikaji Jamii.

Vikao hivyo vya tathmini vilihusisha wadau kutoka nyanda za juu kusini ,  kanda ya ziwa na kanda ya kaskazini.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Bw. Claud Kumalija alielezea jinsi ya kuboresha uwajibikaji jamii katika ngazi za Wilaya, Mkoa na Taifa. Alisema ni muhimu AZAKI kuelewa jinsi serikali inavyofanya shughuli zake za maendeleo na pia ni muhimu kutambua mabingwa wa uwajibikaji wa kijamii ambao watakuwa mstari wa mbele kutangaza ajenda ya uwajibaki jamii ili kuweza kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na AZAKI.

Aidha, Bw. Kumalija alisisitiza kujifunza mbinu za kukusanya nyaraka sahihi za Serikali ili kudumisha uhusiano mzuri kwanzia ngazi ya Halmashauri.

Pamoja na hayo mwakilishi kutoka OR-TAMISEMI, Bi. Mary Shadrack alitoa wasilisho kuhusu Uwajibikaji jamii katika Wizara hiyo kwa kugusia mfano wa Mfumo wa Makole (Makole Model) ambao ulisaidia kuboresha huduma za afya kwa kuainisha changamoto zilizokuwa zikikabili kituo cha afya cha Makole.

Bi. Shadrack alisema kituo cha afya cha Makole kilikuwa na changamoto za kukosa wahudumu wa afya kwa sababu ya utoro, kuwepo kwa viashiria vya rushwa, kutokuwepo kwa vikao vya mipango ambapo changamoto hizi zimesababishwa na ukosefu wa uwajibikaji.

Mfumo wa Makole ulisaidia kuwajengea uwezo wahudumu wa afya kwa kujenga uadiifu na pia wahudumu walijifunza jinsi ya kuimarisha mipango ya uwazi kwa raia ili kupunguza kero zao.

Pia katika vikao hivyo vya tathmini washiriki walipokea mifano ya uwajibikaji jamii kutoka kwa wadau wa AZAKI. Bw. Godfrey Boniventura kutoka HakiElimu alitoa ushuhuda wa jinsi mfumo wa uwajibikaji jamii unavyosaidia kutatua changamoto katika sekta ya Elimu.

Bi Shadrack alisitiza kuwa unaposhirikisha wadau sahihi unapata michango muhimu ambayo inasaidia kutoa muelekeo katika kazi za uwajibikaji jamii kwa kupata mifano halisi katika ngazi mbalimbali.

 

Marejeo ya Mkukuta

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter