Habari Za Hivi Karibuni

Mwanzoni mwa mwaka 2016, Serikali ilizindua FYDP II, kwa lengo la kurekebisha mapungufu ya FYDP I na kutoa mpango makini wakati Tanzania inapoanza kuelekea katika maendeleo ya viwanda katika miaka mitano ijayo (2016 – 2021).

Katika kufanya marejeo ya FYDP I, serikali ilitambua kuwa mpango wa awali ulishindwa kufanikisha malengo yake mengi. Wakati Serikali imedhamiria kuwa ukuzaji wa viwanda ni kipaumbele katika miaka mitano ijayo, mapungufu ndani ya mpango unaweza kufanya nchi ishindwe kwa mara nyingine tena kama masuala yaliyojitokeza hayajafanyiwa kazi vya kutosha.

Majadiliano yaliyopita kati ya Serikali na mashirika binafsi yaliyofanyika mwaka 2016, yaliyolenga kufanyia kazi changamoto na masuala ndani ya FYDP II hayajaleta matokeo yaliyokusudiwa. Ili Tanzania ifanikiwe, mbinu mpya na mawazo mapya yanahitajika haraka. Utekelezaji wa ufanisi wa FYDP II utahitaji uelewa wa ndani wa kwa nini majaribio ya nyuma ya kuimarisha viwanda yalishindwa na kuchukua hatua kuhakikisha kwamba makosa ya nyuma hayarudiwi. Soma zaidi

Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya tathmini ya mwaka na ufuatiliaji wa maendeleo ya utekelezaji wa shughuli zinazogharamiwa na Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa (LGDG) kama zinavyotekelezwa mara kwa mara na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Uhusiano huu unatokana na ukweli kwamba ufuatiliaji unaopaswa kufanywa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa unagusa kwa kiwango kikubwa masuala yaleyale au maeneo muhimu ambayo hufanyiwa tathmini wakati wa upimaji wa mwaka. Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambazo zinafanya jitihada kubwa kufanya ufuatiliaji makini wa programu na miradi yao inayogharamiwa na Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa wanakuwa na nafasi nzuri ya kupata alama za juu kwenye upimaji wa mwaka. Soma zaidi

Serikali imedhamiria kutekeleza Sera ya Ugatuaji wa Madaraka ambapo moja ya mambo ya msingi katika Sera hiyo ni ugatuaji wa masuala ya fedha kupitia eneo hili. MSM zinawezeshwa kifedha kufanya maamuzi yanayohusu maeneo yao ili kukidhi mahitaji yaliyobainishwa kwenye maeneo yao na kutekeleza programu na shughuli zinazotokana na mahitaji hayo. Kwa hiyo, ugatuaji wa masuala ya fedha, una maana kwamba MSM zinawekewa masharti ya kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao kupitia mapato ya ndani na mapato kutoka Serikali Kuu kwa uwazi na usawa. Soma zaidi

Upimaji wa Mwaka wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni zoezi lililoanzishwa na Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa (LGDG) kupima utendaji kazi wa kila Halmashauri kwa kila mwaka ili kuamua kiasi cha fedha cha LGDG ambacho hatimaye kitapelekwa kwenye Halmashauri husika kwa kuzingatia matokeo ya upimaji huo. Soma zaidi

TAMKO LA UMOJA WA WADAU WA HAKI YA KODI TANZANIA (TTJC)

UKUSANYAJI WA MAPATO YATOKANAYO NA RASILIMALI ZA NDANI, MATUMIZI, CHANGAMOTO NA MAPENDEKEZO

Serikali inalo jukumu kubwa la kuwapatia wananchi huduma bora za umma. Ili Serikali iweze kutimiza wajibu wake kwa umma inahitaji rasilimali mbalimbali, zikiwemo fedha. Kushindwa kwa serikali kukusanya mapato ya kutosha kunadhoofisha uwezo wake wa kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba Tanzania inakabiliwa na tatizo la kupoteza kiwango cha juu cha mapato hasa yanayotokana na kodi.

Mnamo mwaka 2012 Kamati ya Viongozi wa Dini ya masuala ya Haki za Kiuchumi na Uadilifu katika Uumbaji walitoa ripoti iliyobainisha, Kiwango cha upotevu wa mapato kuwa Dola za Kimarekani kati ya Milioni 847 na bilioni 1.3. Upotevu huu wa mapato ni kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia misamaha ya kodi na utoroshwaji wa fedha kwenda nje ya nchi

Hali ya sasa inaonesha kuwa upotevu wa fedha za kodi umeongezeka hadi kufikia Dola za Kimarekani Bilioni 1.83, sawa na fedha za Kitanzania takribani Shilingi trilioni 4. Fedha hizi zilizopotea zingeweza kufadhili kwa mara tatu ya bajeti ya Sekta ya Afya, au mara mbili ya bajeti ya Sekta ya Elimu kwa mwaka 2016/17.

Licha ya utafiti uliofanyika mwaka 2017 kuonesha kuongezeka kwa jitihada katika kukusanya mapato, bado serikali inakabiliwa na matatizo kama;

  Ukwepaji wa kodi

  upotevu kwenye misamaha ya kodi

  utoroshwaji wa mali na fedha nje ya nchi.

  Na upotevu mwingine katika manunuzi ya umma

Kuhusu misamaha ya kodi: Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2015/16 inaonesha kuwa Serikali ilitoa misamaha ya kodi ya thamani ya Shilingi trilioni 1.10, sawa na asilimia 1.14 ya pato la ndani la taifa, wakati lengo la Serikali ni kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia chini ya asilimia 1 ya pato la ndani la taifa.

Mkaguzi Mkuu alibaini kuwa misamaha ya kodi imekuwa ikitumika kuwanufaisha watu au makampuni yasiyostahili. Mfano kwa kipindi cha mwaka 2012 hadi 2014, magari 238 kutoka nje ya nchi yaliingizwa nchini kwa kutumia majina ya walipa kodi wawili ambao hawakustahili. Kwa mwaka 2015/16 Serikali ilipoteza shilingi billioni 3.46 kwa kutoa misamaha ya kodi kwa watu wasiostahili.

Kuhusu utoroshwaji wa fedha: Viwango vipya vya upotevu wa mapato yatokanayo na utoroshwaji wa fedha nchini kwenda nje ya nchi ni Dola za Kimarekani milioni 464 kwa mwaka.

Kuhusu manunuzi ya umma: Mwaka 2015/16, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alibaini mapungufu katika utaratibu wa utoaji wa zabuni, na utekelezaji na usimamizi wa mikataba na manunuzi ambayo hayakufanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zake. Kutofuatwa kwa kanuni hizi ni kiashiria kikubwa cha upotevu wa fedha kwa njia badhilifu.

Kuhusu ukusanyaji wa kodi: Imebainika kwamba watu wachache sana, hasahasa walio kwenye sekta rasmi, ndio wanaolipa kodi, hivyo kubeba mzigo wa wale wasiolipa kodi, ambao bado wanafaidi bidhaa na huduma za umma sawasawa na wale wanaolipa kodi.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali 2015/16 inaonesha kuwa takriban Shilingi 588.8 bilioni hazikukusanywa kutoka kwa walipa kodi mbalimbali.

Pia, uchunguzi uliofanyika mwaka 2015 hadi 2016 ulibaini kuwa katika walipa kodi 9,743 waliosajiliwa kukusanya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ni walipa kodi 1,578 ambao ni asilimia 16 tu ndio wanatumia mashine za EFD. Kati ya walipa kodi 49,009 wanaostahili kutumia mashine za EFD ni walipa kodi 9,127, ambao ni asilimia 18.6 tu, wenye mashine hizo.

Mapendekezo: Kupitia kongamano la “Tanzania Extractive Indutries Conference 2017,”Wadau wa Haki ya Kodi Tanzania (TTJC) tunaamini mapendekezo yafuatayo kwa serikali yanaweza kuboresha ukusanyaji na matumizi ya mapato ya fedha za umma.

  Serikali ipunguze misamaha ya kodi

  Iboreshe uwazi katika utoaji wa misamaha ya kodi

  Iendelee kuelimisha wananchi na kuwajibisha wale wote wanaohusika na ubadhilifu, au wanaokiuka sheria zinazosimamia fedha za umma.

  Isambaze na kuonesha umuhimu wa mashine za EFD, na izidi kuwekeza katika mifumo ya kielektronki ya ukusanyaji kodi, hata katika ngazi ya halmashauri

  Na pia itekeleze kwa makini suala la mapitio ya sheria mbalimbali ili makampuni yote yalipe kodi stahiki

  Wananchi watambue kuwa ni wajibu wao kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo yao

Kwa kufanya haya, mapato mengi yataweza kukusanywa, na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kupata huduma muhimu na kwa ubora zaidi.

Tamko hili limeandaliwa na Umoja wa Wadau wa Haki ya Kodi Tanzania (TTJC)
Kwa habari zaidi tafadhali wasiliana nasi: info@policyforum.or.tz

HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (OR-TAMISEMI) MHE. SELEMANI JAFO (MB) WAKATI WA UZINDUZI WA MIONGOZO YA MFUMO WA UTOAJI WA RUZUKU YA MAENDELEO YA SERIKALI ZA MITAA (LGDG) MJINI DODOMA, 28 OKTOBA 2017

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma,

Wenyeviti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Bahi,

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma,

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Bahi,

Mwenyekiti wa Bodi ya Policy Forum,

Wakurugenzi wa Idara na Vitengo OR-TAMISEMI,

Mratibu wa Policy Forum,

Wataalamu kutoka Policy Forum na OR-TAMISEMI,

Waandishi wa Habari,

Washiriki wote Mabibi na Mabwana,

Habari za mchana,

Ndugu washiriki,

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa katika tukio hili muhimu la uzinduzi wa Miongozo ya Mfumo wa utoaji wa Ruzuku ya Maendeleo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM).

Ndugu washiriki,

Miongozo ya mfumo wa utoaji wa Ruzuku ya Maendeleo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa inayozinduliwa leo imeandaliwa na OR-TAMISEMI kwa ufadhili na msaada wa kitaalamu wa Shirika la Policy Forum (PF). Naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana wataalamu wa pande hizi mbili kwa kufanya kazi ya kuitafsiri miongozo hii kwa Lugha rahisi ya Kiswahili, lugha ambayo inaeleweka vizuri kwa wananchi wote hasa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao ndio walengwa Wakuu wa Miongozo hii.

Ndugu washiriki,

Mnamo mwaka 2016, OR-TAMISEMI iliomba msaada wa Policy Forum (PF) wa kuandika kwa lugha rahisi ya Kiswahili na usambazaji wa Miongozo hiyo, ambayo itasambazwa na kutumika katika ngazi za Serikali za Mitaa nchini. Kazi hiyo nimeelezwa imekamilika. Nimeetaarifiwa pia kwamba, Policy Forum waligharamia zoezi hilo, pia wameahidi kuisambaza katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, nawapongeza sana kwa kujitolea kwenu na kuonesha ni kwa jinsi gani mpo nasi bega kwa bega katika kuhakikisha tunaimarisha Serikali zetu za Mitaa ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naomba kuwakumbusha tena kuwa, Miongozo ya Mfumo wa utoaji wa Ruzuku ya Maendeleo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa inajumuisha maeneo matatu muhimu ambayo ni:-

  • Mwongozo wa Utekelezaji na Uendeshaji.
  • Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini;
  • Mwongozo wa Upimaji wa Matokeo kwa Mwaka

Ndugu washiriki,

Jumla ya nakala 33,600 tayari zimeshachapishwa na Policy Forum na baada ya uzinduzi huu, zitasambazwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Nitoe wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zote Nchini kuhakikisha kuwa miongozo hii haiwekwi kwenye makabati, bali inatumika kwa malengo iliyokusudiwa ili iweze kuleta ufanisi katika utendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Naambiwa pia, Policy Forum wako tayari kuchapisha na kuzisambaza nakala nyingi zaidi pindi itakapoonekana zilizopo hazitoshelezi mahitaji. Asanteni sana Policy Forum kwa msaada huo.

Ndugu washiriki,

Napenda pia kupongeza uamuzi mliofikia wa kuwa na Mkataba wa ushirikiano baina ya Policy Forum na OR-TAMISEMI wenye lengo la kurasimisha mahusiano yetu na kupanua wigo mpana zaidi wa kuendelea kushirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili. Ni imani yangu kwamba makataba wa ushirikiano unaotarajiwa kusainiwa mapema iwezekanavyo ili azma yetu ya kuimarisha ushirikiano iweze kutimia.

Ndugu washiriki,

Natumia nafasi hii, kwa mara nyingine kuwatakia kila lakheri katika kudumisha ushirikiano wa kitaalamu na naamini huko tuendako tutaendelea kushirikiana zaidi tukiwa na lengo moja la kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa weledi na uadilifu katika ngazi zote za Serikali za Mitaa ili tuweze kuboresha zaidi utendaji wetu na hivyo kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ndugu washiriki,

Kwa maneno hayo machache, natangaza rasmi miongozo ya Mifumo ya utoaji wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa nimeizindua rasmi. Natoa rai kuanzia leo OR-TAMISEMI na Policy Forum muanze kuisambaza miongozo hii katika Halmashauri zote nchini kama mlivyojipanga.

Asanteni sana

Halmashauri nchini zimeshauriwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili ziweze kupata mapato ambayo yatasaidia katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika ngazi ya serikali za mitaa. Hayo yamesemwa Oktoba 27, 2017 mjini Dodoma na wawakilishi wa idara mbalimbali za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) wakati wa mkutano uliojumuisha wanachama wa Policy Forum (PF) na maafisa wa OR-TAMISEMI.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kukutanisha wanachama wa PF na maafisa wa idara za OR-TAMISEMI kujadiliana namna ya kufanya kazi kwa pamoja hasa katika sekta ambazo zinaweza kuleta mabadiliko katika ngazi ya serikali za mitaa.

Mkutano huo ulitanguliwa na utambulisho wa pande zote mbili ambapo upande wa PF, Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa (LGWG), Kellen Mngoya alitoa usuli kuhusiana na mtandao wa PF na kazi zinazofanywa na vikundi kazi viwili ambavyo ni Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa (LGWG) na Kikundi Kazi cha Bajeti (BWG). Utambulisho wa OR-TAMISEMI ulitolewa na Sebastian Kitiku ambaye ni Mratibu wa Idara TAMISEMI.

Kitiku alianza kwa kutoa utangulizi wa jinsi ambavyo OR-TAMISEMI ilivyoalikwa kwenye mkutano wa wanachama wa PF wa  robo mwaka uliofanyika 2016 na kuomba wanachama wa PF kutumia maarifa na ujuzi wao katika kurahisisha miongozo iliyoandaliwa na OR-TAMISEMI kwa ajili ya matumizi katika ngazi za Serikali za Mitaa nchini.

Kitiku alipongeza juhudi zilizoonyeshwa na wanachama wa PF hasa wa kikundi kazi cha LGWG kwa kuweza kurahisisha miongozo hiyo kuwa katika lugha rahisi. Alitaja miongozo hiyo kuwa ni:

  • Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa: Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini;
  • Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa: Mwongozo wa Upimaji wa Mwaka na
  • Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa: Mwongozo wa Utekelezaji na Uendeshaji.

Wajumbe wa kikao hicho pia walipata nafasi ya kuweza kujadili suala la Serikali Kuu kuchukua baadhi ya vyanzo vya mapato vilivyokuwa vinakusanywa na Halmashauri. Akitolea ufafanuzi juu ya suala hilo Kitiku alieleza kuwa Serikali Kuu iliamua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikusanye kodi katika vyanzo vya mapato vya Serikali za Mitaa kwa kuwa ilionekana Halmashauri hazikuwa na mifumo madhubuti ya kukusanya mapato. Hata hivyo alieleza kuwa zoezi hilo ni la majaribio tu na linafanywa kwenye Halmashauri 30 ambazo ni kubwa ili kupima ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Kitiku alieleza kuwa kwa sasa Serikali ina mpango wa kuboresha upelekaji wa fedha katika ngazi za Halmashauri. Mpango huo umeainishwa vyema katika vitabu vilivyoandaliwa na OR-TAMISEMI na kuandikwa kwa lugha rahisi na kikundi kazi cha PF na vitazinduliwa Oktoba 28, 2017 mjini Dodoma.

Wajumbe wa mkutano huo waliitimisha majadiliano kwa kukubaliana kuwa bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya PF na OR-TAMISEMI. Pia OR-TAMISEMI iliiomba PF iwapatie watumishi wake mafunzo ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ili waweze kutekeleza vyema shughuli zao za usimamizi wa utekelezaji wa SDGs katika ngazi za mikoa na mitaa.

Pia ilipendekezwa kuwa kikundi kazi cha LGWG kiwe kinashirikiana na Idara ya Serikali za Mitaa ya OR-TAMISEMI hasa katika kazi zinazohusiana na mafunzo kwa madiwani au uchambuzi wa sera mbalimbali zinazohusu Serikali za Mitaa, hili lilikuwa pia ni pendekezo litakalohitajika kuonekana kwenye Hati ya Makubaliano. Wajumbe walikubaliana pia kuwa wakati kikundi kazi cha LGWG kikiwa kinatembelea Halmashauri kiwe kinaenda na angalau afisa mmoja kutoka OR-TAMISEMI.

 

 

 

 

Sekta ya nishati inakabiliwa na changamoto mbalimbali hapa nchini ikiwemo: upungufu wa fedha za kutosha, ushiriki na uwekezaji mdogo wa sekta binafsi katika miradi mikubwa ya nishati; utegemezi mkubwa sana kwa tungamotaka kama chanzo cha nishati; gharama kubwa za tozo za uunganishaji na usambazaji wa umeme; upungufu wa wataalam na tafiti; uwepo na matumizi ya teknolojia miundombinu duni; na uwekezaji mdogo katika nishati jadidifu. Soma zaidi...

Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni sekta muhimu sana kwa uchumi na maendeleo ya nchi na Watanzania
kiujumla. Sekta hizi zimeendelea kuwa chanzo kikubwa cha kipato kwa zaidi ya asilimia 65 ya
Watanzania na nguzo muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula, na zinachangia pato la taifa
kwa zaidi ya asilimia 29 na kwa mauzo ya nje zinachangia kwa zaidi ya asilimia 24.
Japo sekta hizi ni muhimu ila zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaathiri ukuaji wake. Soma zadi...

Tanzania (mafuta na gesi asilia): alama za RGI na
vipengele vya upimaji

Sekta ya Mafuta na Gesi asilia ina alama 53 kati ya alama 100 za RGI 2017. Tofauti na sekta ya madini ambayo ni kongwe, Tanzania bado haijaanza uzalishaji mkubwa wa gesi baada ya ugunduzi wa gesi nyingi katika kina kirefucha bahari ya Hindi  ambayo hivi sasa inakadiriwa kuwa futi za ujazo trilioni 57. Hali ya kuridhisha ya Tanzania katika uwezekano wa kupata thamani ya rasilimali, kipengele kinachopima ubora wa utawala katika utoaji wa leseni, mfumo wa kodi, athari kwa jamii na ushiriki wa Serikali, hutegemea sana utaratibu wa kisheria wenye masharti mahimu kuhusu utawala na uwazi. Kwa kuwa Tanzania bado haijaanza uzalishaji mkubwa wa gesi na kuuza nje ya nchi, sheria husika nyingi zikiwa ni mpya hazijatekelezwa kikamilifu kuwezesha tathmini ya ufanisi wake. Kutegemea hali ya uwekezaji na utekelezaji wa sera, sheria na kanuni husika, tasnia ya mafuta na gesi vina uwezo wa kuleta
manufaa makubwa kwa Tanzania moja kati ya nchi zenye ongezeko kubwa la watu duniani. Soma Zaidi ...

Pages

Marejeo ya Mkukuta

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter