Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Halmashauri nchini zimeshauriwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili ziweze kupata mapato ambayo yatasaidia katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika ngazi ya serikali za mitaa. Hayo yamesemwa Oktoba 27, 2017 mjini Dodoma na wawakilishi wa idara mbalimbali za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) wakati wa mkutano uliojumuisha wanachama wa Policy Forum (PF) na maafisa wa OR-TAMISEMI.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kukutanisha wanachama wa PF na maafisa wa idara za OR-TAMISEMI kujadiliana namna ya kufanya kazi kwa pamoja hasa katika sekta ambazo zinaweza kuleta mabadiliko katika ngazi ya serikali za mitaa.

Mkutano huo ulitanguliwa na utambulisho wa pande zote mbili ambapo upande wa PF, Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa (LGWG), Kellen Mngoya alitoa usuli kuhusiana na mtandao wa PF na kazi zinazofanywa na vikundi kazi viwili ambavyo ni Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa (LGWG) na Kikundi Kazi cha Bajeti (BWG). Utambulisho wa OR-TAMISEMI ulitolewa na Sebastian Kitiku ambaye ni Mratibu wa Idara TAMISEMI.

Kitiku alianza kwa kutoa utangulizi wa jinsi ambavyo OR-TAMISEMI ilivyoalikwa kwenye mkutano wa wanachama wa PF wa  robo mwaka uliofanyika 2016 na kuomba wanachama wa PF kutumia maarifa na ujuzi wao katika kurahisisha miongozo iliyoandaliwa na OR-TAMISEMI kwa ajili ya matumizi katika ngazi za Serikali za Mitaa nchini.

Kitiku alipongeza juhudi zilizoonyeshwa na wanachama wa PF hasa wa kikundi kazi cha LGWG kwa kuweza kurahisisha miongozo hiyo kuwa katika lugha rahisi. Alitaja miongozo hiyo kuwa ni:

  • Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa: Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini;
  • Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa: Mwongozo wa Upimaji wa Mwaka na
  • Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa: Mwongozo wa Utekelezaji na Uendeshaji.

Wajumbe wa kikao hicho pia walipata nafasi ya kuweza kujadili suala la Serikali Kuu kuchukua baadhi ya vyanzo vya mapato vilivyokuwa vinakusanywa na Halmashauri. Akitolea ufafanuzi juu ya suala hilo Kitiku alieleza kuwa Serikali Kuu iliamua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikusanye kodi katika vyanzo vya mapato vya Serikali za Mitaa kwa kuwa ilionekana Halmashauri hazikuwa na mifumo madhubuti ya kukusanya mapato. Hata hivyo alieleza kuwa zoezi hilo ni la majaribio tu na linafanywa kwenye Halmashauri 30 ambazo ni kubwa ili kupima ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Kitiku alieleza kuwa kwa sasa Serikali ina mpango wa kuboresha upelekaji wa fedha katika ngazi za Halmashauri. Mpango huo umeainishwa vyema katika vitabu vilivyoandaliwa na OR-TAMISEMI na kuandikwa kwa lugha rahisi na kikundi kazi cha PF na vitazinduliwa Oktoba 28, 2017 mjini Dodoma.

Wajumbe wa mkutano huo waliitimisha majadiliano kwa kukubaliana kuwa bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya PF na OR-TAMISEMI. Pia OR-TAMISEMI iliiomba PF iwapatie watumishi wake mafunzo ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ili waweze kutekeleza vyema shughuli zao za usimamizi wa utekelezaji wa SDGs katika ngazi za mikoa na mitaa.

Pia ilipendekezwa kuwa kikundi kazi cha LGWG kiwe kinashirikiana na Idara ya Serikali za Mitaa ya OR-TAMISEMI hasa katika kazi zinazohusiana na mafunzo kwa madiwani au uchambuzi wa sera mbalimbali zinazohusu Serikali za Mitaa, hili lilikuwa pia ni pendekezo litakalohitajika kuonekana kwenye Hati ya Makubaliano. Wajumbe walikubaliana pia kuwa wakati kikundi kazi cha LGWG kikiwa kinatembelea Halmashauri kiwe kinaenda na angalau afisa mmoja kutoka OR-TAMISEMI.