Mdahalo wa wa asubuhi chini ya mradi wa Raia Makini ulifanyika tarehe 17 Novemba 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi. Lengo kuu lilikuwa kuangazia umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika upangaji wa mipango na bajeti, pamoja na namna Halmashauri inavyotarajia kuwawezesha wananchi kushiriki katika mchakato wa bajeti.
Akifungua mdahalo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Ndugu Philemon Mwita, alitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kuhudhuria vikao rasmi vya vijiji, ambavyo ndiko kunakotolewa maoni, mapendekezo na maamuzi ya msingi kuhusu mustakabali wa maendeleo ya jamii.
Awali, Richard Angelo kutoka Policy Forum alieleza malengo ya mradi wa Raia Makini, unaolenga kuongeza uelewa wa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali za umma na kuhoji uwajibikaji wa viongozi. Mradi huu unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya, ukiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utawala bora barani Afrika. Kupitia ufadhili huo, WAJIBU na Policy Forum wanatoa taarifa sahihi na rahisi kueleweka kuhusu usimamizi wa fedha za umma, ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika midahalo na mijadala ya sera.
Kwa upande wake, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Tanganyika, Bwana Julius Ulaya, alisisitiza umuhimu wa kuoanisha mipango ya maendeleo na sera za kitaifa ili kuakisi vipaumbele vilivyowekwa. Alikumbusha kuwa wananchi wana haki na wajibu wa kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma na kuwawajibisha viongozi pale panapojitokeza matumizi yasiyoridhisha. Aidha, alisisitiza kuwa ujenzi wa Taifa unahitaji ushirikiano kati ya serikali na wananchi.
Mdahalo uliendeshwa na Bwana Nicodemus Luhele, Mkurugenzi wa Taasisi ya TOSOVC, ambaye alitoa fursa kwa washiriki kutoa maoni kuhusu ushiriki wa wananchi katika mchakato wa bajeti na namna ya kuongeza uhamasishaji.
Baadhi ya wananchi kutoka Kijiji cha Mishamo walieleza kuwa mwamko wa kuhudhuria mikutano ya kijiji ni mdogo kutokana na uelewa finyu wa viongozi na wananchi wenyewe. Walitaka elimu endelevu na uwazi katika mchakato wa kupanga bajeti, wakisema baadhi ya mikutano ya maendeleo, ikiwemo ile ya ngazi za vitongoji, haiitishwi kama inavyotakiwa.
Walitoa mfano wa Zahanati ya Kabanga, ambayo imekuwa ikijengwa tangu mwaka 2012 lakini hadi sasa haijamalizika kutokana na changamoto za usimamizi na ushiriki mdogo wa jamii.
Afisa Elimu, Bwana Zabron Kabugu, alieleza kuwa viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa na wanaweza kutumika kuhamasisha jamii, kama inavyoonekana katika miradi ya ujenzi wa nyumba za ibada inayokamilika kwa ubora na kwa muda mfupi. Hata hivyo, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa uwazi wa mapato ya kijiji ili kujenga uaminifu.
Mdahalo ulifikia maazimio yafuatayo:
- Kukutana na uongozi wa kijiji, viongozi wa dini na wazee maarufu ili kuimarisha elimu na uhamasishaji.
- Kutoa elimu endelevu kwa wananchi kuhusu ushiriki katika mchakato wa bajeti na mikutano ya kijiji.
- Kuhakikisha mikutano ya kijiji inafanyika kwa wakati na kufuata taratibu.
- Halmashauri kuongeza ufuatiliaji wa utendaji wa viongozi wa ngazi ya kijiji.
- Kuwatumia viongozi wa dini kuongeza uhamasishaji wa shughuli za maendeleo.
- Kumshirikisha Mkuu wa Makazi kutokana na nafasi yake ya ushawishi (maeneo ya makazi ya wakimbizi).
- Kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika miradi ya maendeleo kuanzia hatua za mwanzo ili kuongeza umiliki wa pamoja.
Mdahalo ulifungwa kwa kusisitiza kuwa maendeleo yanafanikiwa endapo serikali na wananchi watashirikiana, kila mmoja akitimiza wajibu wake kwa uwazi, uadilifu na ufuatiliaji wa karibu.