Kanuni za Maadili ya AZAKI

Rasimu ya Kanuni za Maadili ya AZAKI

Policy Forum, Aprili 2007

Madhumuni ya Kanuni hii ya Maadili ya hiari ni kujenga AZAKI zenye viwango ya juu, bora, zenye manufaa, wenye uwazi na zinazowajibika nchini Tanzania. Sisi, AZAKI za Tanzania na za kimataifa zinazofanya kazi Tanzania, tunakubali kufanya kazi kuhakikisha kuwa sera zetu na utendaji wetu vinaendana na Kanuni hii ya Maadili.[1]

  1.     Imani za msingi

1.1.  Sisi ni asasi huru, zinazojitegemea na zisizofungamana na itikadi yoyote. Tutabuni miradi yetu na kufanya kazi zeti bila msukumo kutoka chama chochote cha siasa, wafanyabiashara au wahisani.

1.2.  Sisi ni asasi zisizo za kiserikali. Tunawajibika kwa malengo yetu wenyewe, imani na vyombo vinavyotuendesha na sio maelekezo kutoka Serikali yoyote, iwe serikali ya mtaa, serikali kuu au serikali ya nchi ya nje.

1.3.  Tunaamini binadamu wote ni sawa. Hatutabagua kwa kigezo cha rangi, kabila, asili ya nchi, jinsia, hisia za kijinsia, ulemavu, hali ya VVU/UKIMWI au hali nyingine yoyote. Badala yake, tutahimiza haki za binadamu, heshima, usawa na ushiriki wa wote, hususan wale ambao kihistoria wametengwa.

1.4.  Tunaamini katika demokrasia shirikishi na tutafanya kazi kuhakikisha sauti na harakati za raia zinapewa nafasi kidemokrasia.

1.5.  Tunathamini maoni tofauti, uhuru wa kujieleza na mjadala wa wazi, na tutaendeleza imani hii katika ngazi zote.

1.6.  Tutajibidisha kufanya kazi kwa ubora na viwango vya juu na kuwa na utamaduni wa kujifunza na kutafakari, katika kila tunalofanya.

1.7.  Tutahimiza uwazi na uwajibikaji katika asasi zetu, ushirika na jamii zetu.

1.8.  Tutaepuka kufanya kazi za kichochezi na zinazodhalilisha serikali kwa njia ya vurugu na mambo yasiyokubalika kikatiba.

 2.     Utawala

2.1.  Tutakuwa na katiba, dira na malengo yanayoeleweka; na tutafanya kazi zetu kufuatana na hayo.

2.2.  Tutakuwa na bodi ya utawala inayoelewa na kukubali majukumu yote ya utawala na kazi zote za asasi. Itatengeneza sera; kupitisha mikakati mikuu/mipango, bajeti na ripoti; na kumsimamia mtendaji mkuu kwa mujibu wa katiba na mamkala ya asasi.

2.3.  Tutafanya Mkutano Mkuu wa Mwaka kwa kutoa taarifa zote na sahihi kuhusiana na mafanikio, matatizo, masuala ya kifedha na utawala.

2.4.  Tutakuwa na taratibu zilizoandikwa kuhusu uteuzi, wajibu na muda wa wajumbe wa Bodi ya utawala na kuonesha mikutano inafanyika mara ngapi, akidi, kuripoti na kazi na mamlaka ya viongozi mbalimbali.

2.5.  Tutatunga na kuzingatia sera inayokataza mgongano wa maslahi wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja kwa wajumbe wa utawala pamoja na wanachama, wafanyakazi  na wanaojitolea kwenye asasi. Wajumbe wa utawala na wafanyakazi hawatashiriki kwenye maamuzi yanayohusu masuala ambamo wana maslahi binafsi au wanaonekana kuwa na maslahi binafsi.

2.6.  Maliza asasi hazitatumika kwa shughuli binafsi mbali na zile zilizoelezwa kwenye katiba au sera zilizoandikwa za asasi.

2.7.  Tutatunga, tutahimiza na kutekeleza sera ya Kutovumilia Rushwa na utovu wowote mkubwa wa maadili katika kila tunachofanya.

 3.     Uwajibikaji

Tunatambua na kujali uwajibikaji kwenye ngazi mbalimbali kama ifuatavyo:

·         Uwajibikaji kwenda chini:  Kwa watu ‘tunaowatumikia’ (‘walengwa’).

·         Kwenye bodi au chombo cha utawala chenye ukubwa sawa kwenye asasi, kwa wafanyakazi wa asasi yetu, kufuatana na sera zetu.

·         Kwa vifungu vya Katiba ya Tanzania na sheria na kanuni nzuri, na kwa wahisani kwa mujibu wa mikataba yetu na uhusiano bora na wahisani

·         Uwajibikaji mlalo:Kwa asasi tunazofanya nazo kazi

 

Tutahimiza uwajibikaji katika mielekeo yote minne, kwa msisitizo maalum kwa uwajibikaji kwenda chini. Tutaepuka kujiingiza sana katika mwelekeo mmoja ambao utatukwaza katika kutimiza mwelekeo mwingine. Katika hili:

 

3.1.  Tutawasiliana mara kwa mara, katika njia rahisi na inayoeleweka, kuhusu imani yetu, muundo wetu wa uongozi, dira, malengo, mtindo wetu wa kufanya kazi na maendeleo tuliyofikia.

3.2.  Tutatengeneza programu ambazo matarajio yake (matokeo) yameelezwa bayana.

3.3.  Tutapanga bajeti ambayo inaendana na kazi na mipango yetu

3.4.  Mara kwa mara tutafuatilia, kuchukua kumbukumbu na kuripoti kuhusu maendeleo ya kazi zetu dhidi ya mipango na bajeti iliyopangwa.

3.5.  Tutahimiza njia zinazotekelezeka ambapo watu waliohusishwa au wanaoathiriwa na kazi zetu wanaweza kuwasiliana nasi na kutuletea taarifa na mrejesho nasi tutauzingatia kwa makini.

3.6.  Tutahimiza sera na utendaji unaoleta uendelevu wa maliasili na mazingira, na zinazoepusha uharibifu wa mazingira.

3.7.  Tathimini ya mara kwa mara itakayoangalia, pamoja na mambo mengine, ubora na manufaa ya kazi zetu.

3.8.  Tutatengeneza na kuitoa kwa umma Taarifa ya Mwaka inayoeleza wajumbe wa Bodi, malengo makuu, matatizo, na mambo tuliyojifunza katika kutekeleza kazi zetu; pamoja na mapato ya mwaka, matumizi na salio.

3.9.  Tutajenga na kutekeleza utamaduni wa tathimini tunduizi, tafakari na kujifunza, na kueleza jinsi tunavyotumia uzoefu tuliopata kuboresha kazi zetu.

 4.     Rasilimali Watu

Waajiriwa na wafanyakazi wa kujitolea ndiyo moyo wa asasi yoyote. Kwa hiyo:

4.1.  Tutatengeneza na kufuata kanuni za sera iliyoandikwa ya rasilimali watu na utawala ambayo itakuwa inaeleweka, na inaendana na sheria za Tanzania.

4.2.  Tutahimiza na kutumia usawa na kutobagua katika kuajiri kwa kiwango kikubwa itakavyowezekana kufuata usawa wa kijinsia katika idadi ya wafanyakazi.

4.3.  . Tutajibidisha kutengeneza mazingira mazuri ya kazi, ambapo kuna kuheshimiana na ambapo hakuna kuvumilia udhalilishaji wa kijinsia na vitendo vingine vinavyovunja heshima ya wafanyakazi.

4.4.  Tutaanzisha utaratibu wa kueleza kutoridhishwa na jambo na utaratibu wa kuchukua hatua za kinidhamu

4.5.  Tutahimiza kujiendeleza kwa asasi na wafanyakazi, na kujenga utamaduni wa kujifunza kutokana na makosa, uwazi, ubunifu, na ugunduzi.

4.6.   Tutatunga sera ya kuzuia mgongano wa maslahi, ukabila, upendeleo na rushwa, pamoja na kulinda watoa-taarifa.

 5.     Uwazi wa Kifedha na Uwajibikaji

5.1.     Tutatengeneza na kutumia kanuni za fedha zilizoainishwa vizuri zinazoonesha kiwango cha juu cha maadili na ambazo zinaendana na kanuni za usimamizi mzuri wa fedha.

5.2.     Tutajitahidi kupunguza matumizi katika utafutaji fedha na utawala kwa kiwango kinachowezekana, ili kiwango kikubwa cha fedha kitumike katika miradi.

5.3.     Tutasimamia rasilimali kwa busara na kwa njia ambazo zinaleta thamani kwa fedha, ikiwa ni pamoja na kuajiri wafanyakazi wenye uwezo kusimamia rasilimali hizo.

5.4.     Tutahakikisha kuwa nyendo zote za fedha ziko wazi na zinarekodiwa vizuri na kwamba nyaraka zake zinahifadhiwa kwa miaka kadhaa kama taratibu za kifedha zinavyotaka.

5.5.     Tutahakikisha kuwa matumizi yoyote makubwa ya fedha yanaidhinishwa baada ya kuchunguzwa na ofisa zaidi ya mmoja, na kwamba mtendaji mkuu au ofisa yoyote hawi na mamlaka yasiyo na mipaka.

5.6.     Tutahakikisha kuwa manunuzi yanafanyika kwa njia ambayo inahakikisha gharama kidogo na kuepuka upendeleo na rushwa, na kwamba yako wazi na yamerekodiwa na yanaendana na masharti ya kanuni za manunuzi.

5.7.     Tutakuwa na rejesta ya vifaa kwa mujibu wa kanuni za kihasibu

5.8.     Tutaendesha akaunti ya benki katika taasisi ya fedha iliyosajiliwa ambamo fedha zote zitawekwa.

5.9.     Tutatunga na kufuata sera wazi kuhusu posho, malipo ya kazi ya kitaalam, zawadi na malipo mengine kuepuka mgongano wa maslahi kupingana na vipaumbele vya asasi na kwa ajili ya uwazi na haki.

5.10.Tutaandaa taarifa ya fedha iliyokamilika ambayo inaeleza bayana mapato (kutoka vyanzo vyote), matumizi na salio, pamoja na ulinganisho wa matumizi halisi dhidi ya bajeti, kwa mujibu wa taratibu za uhasibu.

5.11.Wakati mapato yetu ya mwaka ni zaidi ya Tsh milioni 50, tutahakikisha kuwa hesabu zetu zinakaguliwa na mkaguzi wa hesabu aliyesajiliwa, na kwamba tutatekeleza mapendekezo ya mkaguzi wa hesabu.

5.12.Hatutavumilia rushwa hata kidogo na njia nyingine za matumizi mabaya ya fedha, na tutachukua hatua kali na kumwajibisha mtu atakayehusika na hayo.

 6.     Utekelezaji Endelevu wa Kanuni ya Maadili

Tutaendelea kujitahidi kuimarisha na kuboresha uzingatiaji wetu wa kanuni hii ya maadili, kwa hiyo tutafanya yafuatayo:

6.1.  Kwa uwazi na kwa makusudi kuweka mikakati ya kutimiza viwango vilivyotajwa katika kanuni hii.

6.2.  Tutahimiza na kuendeleza mazingira mazuri yanayowezesha utamaduni wa mtu mmoja mmoja , kikundi, na asasi kujifunza muda wote ndani ya asasi yetu na kwa kushirikiana na asasi nyingine.

6.3.  Tutajihusisha katika tathimini endelevu ya mtu binafsi, wenzako na watu wa nje ili kufuatilia maendeleo ya asasi yetu.

6.4.  Mara kwa mara tutakuwa tukitoa taarifa ya maendeleo tuliyofikia katika kufuata kanuni hii ya maadili 

Imesainiwa:

Jina la Mtendaji Mkuu      

Asasi           

Tarehe

1.2.


[1]Rasimu hii imetengenezwa baada ya kupitia kanuni za maadili za nchi kadhaa, na kanuni za awali zilizotengenezwa na mashirika na washauri wataalam nchini Tanzania

Undefined

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter