Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Sisi Waheshimiwa madiwani tulioshiriki warsha ya mafunzo ya uongozi na uwajibikaji wa kijamii iliyoandaliwa na kuratibiwa na Kinkundi kazi cha Serikali za Mitaa cha Policy Forum kwa kushirikiana na halmashauri ya Kiteto kati ya tarehe 18 hadi 23 Julai 2016,

Baada ya kupokea na kujadili mada mbalimbali, tumetambua umuhimu wa nyaraka na taarifa mbalimbali kwenye hatua zote za usimamizi wa rasilimali za umma na mfumo wa uwajibikaji jamii,

Kwa kuwa tumetambua ukweli kwamba kuna changamoto kubwa ya kupata nyaraka muhimu na za msingi za uendeshaji wa halmashauri kama vile Mpango Mkakati (Strategic Plan), Mpango wa Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF), Mwongozo wa Usimamizi wa Fedha wa Serikali za Mitaa na nyaraka nyinginezo zinazohusika, 

Baada ya kugundua mapungufu ya mchakato wa uandaaji wa bajeti na uduni wa ushiriki wa wananchi,

Baada ya kugundua kuwa rushwa ni adui mkubwa wa haki na inalemaza msukumo wa maendeleo na kutimiza haki kwa wananchi kwa mujibu wa katiba na mikataba ya kimataifa, 

Kwa kuwa tumeona umuhimu wa sisi kama wawakilishi wa wananchi kudai ufafanuzi, uhalali na uthibitisho juu ya maamuzi, mipango na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za halmashauri vinavyofanywa na watendaji wa halmashauri na mamlaka zilizo juu ya baraza la madiwani,

Kwa kutambua nafasi yetu na majukumu yetu kama viongozi na wawakilishi wa wananchi tumeamua kupendekeza na kuazimia yafuatayo;

  1. Policy Forum iandae utaratibu kwa kuwashirikisha wanachama wake waliopo wilayani kiteto hususan KCS kufanya mafunzo ya uwajibaki jamii katika ngazi za chini zaidi za serikali za mitaa (kata na vijiji)
  2. CMT iongeze bidii kuwapatia waheshimiwa madiwani nyaraka zinazopatikana ngazi ya halmashauri na pia Policy Forum iwezeshe upatikanaji wa nyaraka zilizoko ngazi ya taifa na kuwapatia madiwani machapisho mbalimbali yaliyo katika lugha rahisi.
  3. Sisi kama wajumbe wa baraza la madiwani tumeamua kuanzia sasa kuhakikisha tunaleta mabadiliko katika ufanisi wa halmashauri yetu kwa kusimamia utawala bora na uwajibikaji wa kijamii ikiwemo kuhoji na kushauri mamlaka za utendaji zilizo chini yetu ili kuleta matokeo makubwa kwa misingi ya uadilifu na uwajibikaji.
  4. Tutasimamia na kutoa ushauri kwa watendaji wa halmashauri ili kuboresha mchakato wa kuandaa mipango na kutenga rasilimali za kutosha ili wananchi wawe wanapata haki na kunufaika na rasilimali za umma.
  5. Tutahakikisha tunatimiza wajibu wetu katika uendeshaji wa halmashauri ya Kiteto ikiwemo kuhimiza kuwa na rasilimali watu ya kutosha na wenye utalaamu, ujuzi na uzoefu wa kutimiza majukumu yao.
  6. Watendaji wa halmashauri katika ngazi zote kwa kuratibiwa na mkurugenzi mtendaji ambaye ni katibu wa baraza waandae taarifa za utekelezaji na kuweka mfumo wa kuwa na taarifa moja itakayosomwa mbele ya baraza la madiwani kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa, pendekezo hili limejengeka kwenye muktadha wa kuitaka serikali iache utaratibu wa kuwafanya madiwani kuwa ndio wasomaji wa taarifa za utekelezaji jambo ambalo linapunguza hadhi ya chombo cha kufanya maamuzi na kusimamia uwajibikaji (oversight body).
  7. Tutasimamia uadilifu na vita dhidi ya rushwa katika kutimiza majukumu yetu ili kuwa na halmashauri ya kupigiwa mfano katika utawala bora na uwajibikaji wa kijamii.
  8. Mafunzo haya kurudiwa mara mbili au tatu ili kuimarisha uelewa wa madiwani.
  9. Watendaji wa halmashauri wawe tayari kutoa mrejesho kwa Policy Forum juu ya utekelezaji wa haya mafunzo.